JPM ajibu mapigo


*Ni kuhusu kutohudhuria Mapinduzi Zanzibar
*Uamuzi wake wa kununua ndege 6 za ATCL

Mwandishi Wetu

Dk. John Magufuli
NI kama amebadili gia angani. Rais John Magufuli jana aliufanya mkoa wa Shinyanga kuwa wa kwanza kufanya sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar ndani ya Tanzania Bara huku akieleza sababu za kufanya hivyo, akizima minong’ono na hoja zilizozuka zikihoji sababu za yeye kutohudhuria sherehe hizo visiwani.

Aidha, Dk Magufuli alitumia sherehe hizo za miaka 53 ya Mapinduzi, kumjibu Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuhusu lawama dhidi ya kununua ndege badala ya kuondolea wananchi shida ya maji.

Akihutubia wananchi kwenye uwanja wa Kambarage Shinyanga Mjini, Rais Magufuli alisema aliamua kufanya sherehe za Mapinduzi Shinyanga na kwamba kuanzia sasa sherehe zote za kitaifa zitakuwa zikisherehekewa katika kila mkoa nchini.

Rais Magufuli alisema wakati yeye akifanya sherehe hizo mkoani humo, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein amempa Waziri wa Tamisemi Zanzibar, Haji Omari Kheir ili kusherehekea sikukuu hiyo kama ilivyofanyika Zanzibar.

“Tunataka Mapinduzi yanufaishe wananchi wote wa Tanzania kwa vitendo. Kwani kuna ubaya gani Mapinduzi yakisherehekewa Zanzibar na Tanzania Bara, hakuna ubaya mtu akiwa na ‘bethidei’ ikasherehekewa Zanzibar, ikasherehekewa pia Dodoma, zote ni sherehe.

“Watu wamezoea kila sherehe tujirunde sehemu moja wakati tunaweza kutawanyika kila kona ya nchi hii na bado tukasherehekea sikukuu yetu bila kuondoa maana iliyokuwapo mwanzo,” alisema Rais Magufuli.

Alisema Mapinduzi yaliyofanyika Zanzibar miaka 53 iliyopita, ndiyo yamesababisha kuwepo kwa Tanzania ya sasa, huku yakiwezesha pia Waziri wa Ujenzi, Profesa Makame Mbarawa anayetoka Pemba kuwa Waziri.

Rais Magufuli pia alitumia fursa hiyo kumtupia kijembe, Lowassa ambaye aligombea urais kupitia Chadema na kushindwa kwenye Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka juzi.

Katika mikutano yake ya ndani, Lowassa ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema alinukuliwa na vyombo vya habari akiponda hatua ya Rais kununua ndege mbili aina ya Bombadier, akisema alipaswa kutengeneza miundombinu ya maji kwanza badala ya kununua ndege.

Lakini jana akijibu hoja hiyo, bila kutaja jina la Lowassa, Rais Magufuli alisema: “Wapo watu wamekuwa wakiponda kila jambo ambalo Serikali inafanya, fikirieni tulikuwa hatuna ndege hata moja ya Serikali, lakini leo tuna mbili lakini kuna watu wanasema tungeleta maji, wakati yeye alikuwa Waziri husika na bado shida ya maji imeendelea kuwapo.”

Akizungumzia elimu, Rais Magufuli alisema uamuzi wa Serikali kutoa elimu bure umechangia kuongeza idadi kubwa ya watoto wanaosoma ambapo kwa mwaka uliokwisha, watoto waliojiunga na elimu ya msingi walikuwa milioni mbili tofauti ya milioni moja mwaka juzi.

Rais pia alizungumzia elimu ya juu ambapo alisema Serikali imefanikiwa kutoa mikopo kwa wanafunzi kulinganisha na miaka ya nyuma ambapo mwaka jana kiasi cha Sh bilioni 500 zilitengwa kwa wanafunzi 120,000 sawa na asilimia 100 kulinganisha na Sh bilioni 373 zilizotengwa kwa mwaka juzi kwa wanafunzi 85,000.

Kuhusu vita dhidi ya mafisadi, Rais Magufuli alitaka Watanzania kuendelea kumwombea kwani kazi hiyo bila mkono wa Mungu ni ngumu, huku akisisitiza kuwa anataka kuona masikini wakiishi kama malaika huku waliozoea ‘kupiga dili’ wakiishi kama mashetani.

“Najitoa sadaka kwa ajili yenu na hii ni kwa sababu watu walikuwa ‘wakipiga dili’ na kunufaisha matumbo yao kwa fedha za maendeleo hivyo niwahakikishie kuwa Serikali ya Magufuli itapambana na kuhakikisha hakuna watu wanatumia fedha za Watanzania kujinufaisha,” alisema.

Alitaka Watanzania kufanya kazi na kuacha kulalamika kuwa fedha mifukoni zimekwisha na kusema wanaolalamika ni waliokuwa wakitegemea fedha za ‘dili’ huku akiwauliza kuwa “kwani hapo mwanzo zilikuwa zikigawiwa bure?”.

Wadau

Mapema wadau mbalimbali walitofautiana kuhusu hatua Rais Magufuli kutohudhuria sherehe hizo.

Baadhi walisema hakuna tatizo kwa yeye kutohudhuria sherehe hizo, huku wengine wakisema kwa kuwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania aliwajibika kwenda.

Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chauma), Hashim Rungwe alisema haikuwa na umuhimu wa yeye kuwapo kwani si mgeni rasmi wa sherehe hizo na kubainisha kuwa hatua hiyo isingeathiri chochote.

“Yeye hana mizinga pale wala chochote, sioni mahala popote ambapo amekosea sana, hata asipokwenda haina madhara, si mgeni rasmi kwamba asipokuwepo sherehe haifanyiki, yeye akienda ni kama mimi tu,” alisema Rungwe.

Aidha, alisema kukosekana kwake labda ni kujivunija heshima kwa hadhi yake kama Rais wa Jamuhuri ya Muungano ambapo alisema masuala yote yanayohusu Muungano angetakiwa kushiriki.

Rungwe aliongeza kuwa Rais Magufuli huhitajika Zanzibar inapokuwa katika tishio kama la kuvamia au kupoteza Dola kwa kuwa yeye ndiye Amiri Jeshi Mkuu hivyo kuwajibika kutuma majeshi.

Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Danda Juju alisema tafsiri yake ni umuhimu wa sherehe zenyewe, akibainisha kuwa sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar ni mapindunzi ambayo kimsingi yalilenga kujitawala.

“Sasa hili tukio ni kubwa sana la kihistoria, kitendo cha Rais kushindwa kupima umuhimu wa hivi vitu na kuheshimu kumbukumbu kujua tulitoka wapi ni kitendo ambacho kinaonesha kuwapo changamoto kwenye uongozi,” alisema Juju.

Alieleza kuwa kutokana na umuhimu wa tukio hilo, alitakiwa kuwa mfano wa kuheshimu Mapinduzi hayo kwa kutambua “tulikotoka na tunakoelekea”.

Katibu Mkuu wa National League for Democracy (NLD), Tozi Matwanga alisema hajui Rais ataliambia nini Taifa kwa kutohudhuria kwani ni sawa na kuonea Wazanzibari.

“Kwa kitendo hicho ameonea Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla, kwa sababu yeye ndiye mhimili wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema Matwanga.

Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alisema hajui sababu ya Rais kutokwenda kwenye maadhimisho hayo.

“Siwezi kujua labla huenda ana nyingi au anaumwa, hivyo mwulizeni kwanza Msigwa (Gerson) aseme kwa nini hajaenda ndiyo uniulize mimi,” alisema Lissu.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo