IMF yaagiza fedha ziachiwe


*Yapongeza ukuaji uchumi, ukusanyaji mapato, vita dhidi ya rushwa
*Yataka sekta binafsi ishirikishwe utekelezaji wa sera za Serikali

Mwandishi Wetu

Rais John Magufuli
SHIRIKA la Fedha la Kimataifa (IMF), limeitaka Serikali ya Tanzania, kulegeza masharti ya mzunguko wa fedha kwa kuuongeza kupitia kuimarisha sekta binafsi, ili kujenga msingi wa uhakika wa kuendelea kukua kwa uchumi wa nchi.

Taarifa ya Ofisa Habari kutoka Idara ya Mawasiliano ya IMF, Andrew Kanyegirire, iliyowekwa kwenye mtandao wa Shirika hilo jana, ilieleza kuwa tamko hilo lilitolewa baada ya kukamilika kwa kikao cha Bodi ya Utendaji ya Shirika hilo, kilichofanya mapitio ya tano ya uchumi wa Tanzania.

Tamko hilo la IMF, linaipongeza Serikali kwa kuimarisha uchumi, kudhibiti mfumuko wa bei, kupunguza pengo linalotokana na ununuzi nje ya nchi, ikilinganishwa na mauzo   ya nje na kufikia vigezo vya malengo ya kiuchumi kupitia utekelezaji wa sera zake.

Hata hivyo, IMF ilionya kuwa ukuaji mzuri wa uchumi ulioonekana katika nusu ya kwanza ya mwaka jana, uko hatarini kuwa endelevu kutokana na ubanaji wa mzunguko wa fedha.

Pongezi
IMF ilisema uchumi mpana wa Tanzania uliendelea kuimarika na ukuaji wake kuwa katika viwango vinavyoridhisha katika nusu ya kwanza ya mwaka jana na unatarajiwa kukua kwa asilimia saba kwa sehemu iliyobaki ya mwaka.

Shirika hilo lilipongeza kudhibitiwa kwa mfumuko wa bei, uliofikia chini ya malengo ya asilimia tano na vipimo vikionesha kuwa mfumuko huo utaendelea kuwa katika kiwango kinachoridhisha katika nusu ya mwaka iliyobaki.

Pia liliridhishwa na namna pengo linalotokana na matumizi ya fedha za kigeni katika ununuzi wa mahitaji ya Taifa kutoka nje ya nchi, ikilinganishwa na mauzo ya Taifa katika soko la kimataifa, lilivyopunguzwa kutokana na kupungua kwa ununuzi wa huduma na bidhaa za nje ya nchi.

Shirika hilo pia lilieleza kuwa pamoja na utekelezaji wa baadhi ya sera kuwa wa kusuasua, lakini Serikali hivi karibuni ilifanyika kazi utekelezaji wa baadhi ya sera, zikiwamo hatua zilizochukuliwa katika makusanyo wa fedha za umma, kudhibiti deni la Taifa, kuboresha mfumo wa sera ya fedha na kuboreshwa kwa usimamizi wa mashirika ya umma.

Pongezi zingine zilielekezwa kwenye utekelezaji wa ajenda ya mabadiliko katika uchumi kama ilivyoelezwa katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano na mapambano dhidi ya rushwa na kuzuia uvujaji wa mapato ya kodi, ambavyo viliongeza mapato ya Serikali.

IMF ilieleza kuwa kama mapambano hayo yatakuwa endelevu, Taifa litakuwa limejijengea matarajio ya uwekezaji mkubwa katika miundombinu kuanzia utekelezaji wa Bajeti ya 2016/17.

Shirika hilo pia lilielezea mafanikio ya aina yake katika kubana matumizi, yaliyofikisha Serikali kupata bakaa ya fedha kati ya Julai na Septemba, baada ya kukusanya mapato na kudhibiti matumizi, kuwa itasaidia kuwekeza kwenye miradi ya umma na kuvutia mitaji kutoka nje ya nchi.

Pia lilipongeza ongezeko la mapato ya fedha za kigeni lililoonekana tangu mwanzo wa mwaka wa fedha ulioanza Julai mwaka jana.

Hadhari
Pamoja na mafanikio hayo, IMF ilionya kuwa Taifa linakabiliwa na hatari itakayozuia kuendelea kukua kwa uchumi kutoka sekta binafsi.

“Kuna hatari ambayo inaweza kuathiri ukuaji wa uchumi kusonga mbele, inayotokana na masharti magumu ya mzunguko wa fedha, ukuaji unaosuasua wa utoaji mikopo unaoonekana kuwa endelevu, utekelezaji unaosuasua wa miradi ya maendeleo na mtazamo wa sekta binafsi wa kutojiamini kuhusu mikakati mipya ya kiuchumi ya Serikali,” ilieleza taarifa hiyo.

Kutokana na hatari hiyo, IMF ilishauri masharti magumu ya mzunguko wa fedha yaliyopo yalegezwe kupitia sera za fedha za muda mfupi, zitakazotekelezwa kwa nia ya kutimiza malengo ya kiuchumi.

IMF ilitaka ulegezaji huo wa masharti ya mzunguko wa fedha, uendane na msukumo wa kuongeza mikopo kwa sekta binafsi na kushauri Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ichukue hatua hizo wakati Serikali nayo ikianza kuwekeza kwenye miradi ya umma.

“Kuhusishwa kwa ukamilifu wake kwa wadau wote katika uundaji na utekelezaji wa sera, ikiwemo umuhimu wake sekta binafsi, ni muhimu,” ilisisitiza taarifa hiyo.

Umuhimu wa ushauri
Kikao hicho cha mapitio ya uchumi, ni sehemu ya Mfumo wa Kusaidia Utekelezaji Sera (PSI) chini ya IMF ambao taarifa zake hutumiwa na wabia wa maendeleo, nchi wahisani, benki za kimataifa za maendeleo na masoko ya mitaji inayoshiriki maendeleo ya nchi husika.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo