Mokiwa: Mgogoro Anglikana ni wa kuchonga


Salha Mohamed

Dk Valentino Mokiwa
ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk Valentino Mokiwa, amesema mgogoro katika Dayosisi hiyo ni wa kutengenezwa na hauna uhalisia.

Mokiwa alisema hayo jana, siku moja baada ya Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Dk Jacob Chimeledya kudai kumng’oa madarakani.

“Mambo mengi ya kutengenezwa, yametengenezwa huko baa Sinza na kusainiwa barabarani humo. Mimi mwenyewe Desemba 18 mwaka juzi niliwaita watu hawa nikae nao lakini walikimbia,” alisema Mokiwa.

Hata hivyo, alipotafutwa jana kuzungumzia kauli ya Mokiwa, Askofu Mkuu Chimeledya ambaye alinukuliwa akisema iwapo Askofu huyo atasema lolote, yeye (Askofu Mkuu), ‘atamwaga mboga’ alisema:

“Sipo tayari kuendeleza malumbano wala mgogoro. Mimi nilishatoa taarifa yangu imetosha, pale kwamba anaipokea au haipokei, andikeni alichosema lakini sitaki kutoa mawazo katika aliyosema.”

Alisema taarifa yake ilishasema na hawezi kurudia, hivyo muhimu si mabishano bali maisha ya waumini na haitakuwa hekima viongozi kugombana huku vyombo vya habari vikiandika.

“Andikeni alichosema yeye, mimi sitaki kusema chochote, lakini kwa afya ya Kanisa sitaki kulumbana kwenye vyombo vya habari,” alisema.

Aliwataka waumini watulie na wapo watakaopima mambo na kuona au kuelewa nini kinaendelea, huku akibainisha kuwa Kanisa halitakufa.

“Kanisa litaendelea, halifi leo….halifi, ila tunaweza tukachochea watu wakapigana kwa kutumia njia zisizo sahihi na mimi nilishasoma barua na ujumbe ulifika inatosha,” alisema.

Hata hivyo, Mokiwa alieleza kumshangaa Askofu Mkuu kufika wakati wa kikao cha Halmashauri ya Kudumu akiwa na askari wenye sare takribani 12 huku ikiwa ni mara ya kwanza kukutana na Halmashauri ya Dayosisi hiyo.

“Alitushangaza akiwa na ujio wa askari 12 waliovaa sare, kilichomleta ni jambo aliloliita kuwa mrejesho, lakini aliishia kusoma barua ya kudai ameniondoa kwenye madaraka ya huduma ya uaskofu.

Alisema baada ya Askofu Mkuu kutoa kauli hiyo, Halmashauri ya Kudumu ya Dayosisi hiyo ambayo Askofu Mkuu hakuwahi kukutana nayo, haikukubaliana naye.

Mokiwa alisema Halmashauri ya Kudumu haikuwahi kupeleka mgogoro au machafuko ya Dayosisi hiyo kwani Askofu ndiye anafanya kazi na Halmashauri hiyo.

Alisema Askofu Mkuu Chimeledya amekuwa na makundi anayofanya nayo kazi bila kufuata utaratibu wa Kanisa.

“Kwa nini Askofu Mkuu kufanya kazi na watu ambao si sehemu ya mamlaka halali ya Dayosisi ya Dar es Salaam? Halmashauri ya Kudumu ilimwambia kuwa aliyozungumza kwenye kikao hicho ni batili na wana Askofu mmoja ambaye ni Mokiwa,” alisema.

Alisema alichozungumza kwenye kikao cha Halmashauri ya Kudumu kina upungufu kwani hapaswi kuwa nje ya Nyumba ya Maaskofu  na kufanya kazi nje ya taratibu zao.

Askofu Mkuu ana timu yake ya maofisa, lakini katika hili walimshauri vibaya, vyote vimekosewa katika kusimamia taratibu zake.

Mokiwa alisema Askofu Mkuu, hakuingia kwa mujibu wa taratibu na usimamizi na uendeshaji wa Kanisa hilo “Dayosisi ya Dar es Salaam haina mgogoro na mimi ndiye Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Dar es Salaam, mgogoro wanaosema ni wa kutengenezwa,” alisisitiza.

Alisema kutokana na hayo yote anaweka msimamo wa kuwa yeye ndiye Askofu wa Jimbo hilo, ingawa yaliyofanywa ni magumu kwake, huku yakisemwa vibaya.

“Wale ni binadamu na kazi yangu mimi ni kuwaombea nami nimewasamehe na sina tatizo na yeyote katika wao, huo ndio msimamo wangu,” alisema.

Aliomba msamaha kwa jamii ya Anglikana na wana imani nchini kwamba taasisi za dini hazipaswi kufanya mambo ya aina hiyo kwani ni aibu.

Mokiwa alisema bado wanahitaji kujenga umoja na kuondokana na migogoro ya kutengeneza na vita ya kuwaaibisha hivyo makanisa na waumini watulie.

“Niwahakikishie wananchi kuwa hakutakuwa na mgogoro wowote mimi ni Askofu wa Dar es Salaam sijaomba msaada wa polisi katika mizunguko yangu, sijalindwa wala kula chakula mahali kokote, nina imani na wananchi wa Dayosisi, kwamba tukisimama pamoja tutayashinda,” alisema Mokiwa.

Mbali na maelezo hayo, Mokiwa alitaja aliodai walitengeneza mgogoro na kusababisha yeye kufukuzwa kuwa ni Mshauri wa Askofu Mkuu, Makamu wa Askofu Mkuu, Dayosisi ya Newala, Katibu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania ambaye pia ni Padri kwenye Dayosisi ya Morogoro.

“Hapa Dar es Salaam Askofu wetu mkuu anafanya kazi na Kanisa la Andrea Mtakatifu Magomeni, ambako kuna mtu tulimwondolea haki ya kisakramenti, baada ya kukiuka utii kwa kugoma kuhama,” alisema.

Mokiwa alimtaja mwingine kuwa ni aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Uinjilisti, Utume katika Dayosisi hiyo ambaye pia alimtoa kutokana na mambo ya kifedha na uaminifu kwa kujikopesha kutoka Saccos ya Kanisa.

Mokiwa alisema mtu huyo aliondolewa kwa alichodai kuwa ni utapeli baada ya kukopa na kukimbia kulipa madeni katika Benki ya Afrika (BOA), Benki ya Akiba na Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB) kwa kutoa picha zake.

“Sikutaka kuzungumza wakati wowote, lakini sasa imebidi niseme kwa hao wanaotumika na Jimbo.  

“Kanisa letu lilishawahi hata kuandikiwa na Serikali kuwa linaongoza kwa migogoro ambayo mingi ni ya kutengeneza, ili kusiwepo maelewano baina ya waumini na Askofu ili kusitawalike na wakubwa waingie kushika hatamu hapa, hilo tunalijua,” alisema Mokiwa.

Alisema uongozi wa Kanisa umeingia kufanya kazi kando ya utaratibu na kuleta maumivu kwa kumgonganisha Askofu na watu anaowaongoza.

Alisema uongozi wa Kanisa uliingia maeneo mbalimbali na kusababisha maumivu kwenye Dayosisi ambapo alibainisha kuwa Askofu Mkuu hafuati utaratibu.

Alisema watu hao ndio walitumiwa na Askofu Mkuu kwa kutengeneza mashitaka ya Dayosisi hiyo, huku akithibitisha kuwa maaskofu hao kutumika kukusanya saini ambapo watatu walikiri kulaghaiwa na kusaini bila kufahamu.

Mokiwa alisema Desemba 18 mwaka jana alikwenda kusali katika Kanisa la Ubungo ambako ilikamatwa barua pepe yenye mazungumzo kati ya Katibu Mkuu, akiwasiliana na makundi ya Dayosisi ya Dar es Salaam kutoa siri za ofisi.

“Kanisa la Magomeni halijawahi kushindwa kugombana na Askofu mwingine yeyote katika Dayosisi hii, watagombana hadi na maaskofu 27 waliobaki,” alisema.

Alisema hiyo ni roho ya vita inayozunguka ndani yao, huku akibainisha kuundwa kwa Tume ya Askofu inayotumia gari la Serikali namba STK 2948 mkoani Singida.

“Sisi tunafahamu Kanisa lile gari lipo linafanya kazi za mkoa wa Singida linaingiaje kufanya kazi ya Kanisa?” Alihoji akisema haliko kwenye mamlaka ya Kanisa.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo