Mufti ataka Taifa liombewe mvua


Celina Mathew

BAA la njaa linaloikumba nchi limemuibua Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir ambaye amewataka viongozi mbalimbali wa dhehebu la Kiislamu kufanya maombi maalumu kwa ajili ya taifa.

Akizungumza Dar es Salaam kwa niaba ya Mufti, Mwenyekiti wa Halmashauri kuu Bakwata Taifa, Sheikh Khamis Mataka alisema kumekuwa na matamko mbalimbali yanatolewa kuhusu baa la njaa, hivyo kwa kiasi kikubwa dua hiyo itasaidia.

“Nawataka wahusika wote kuleta maombi ya toba ili tuweze kumwomba Mungu msamaha na aijalie nchi yetu na jirani kupata mvua za kheri zitakazosaidia kutuepusha na ukame na madhara mengine, ikiwemo baa la njaa,” alisema Mufti huyo.

Wakati huohuo, Mufti Zubeir amewateua Sheikh Mataka na Mkurugenzi wa Daa’wa na Tabligh Bakwata kuwa wasemaji wa baraza hilo na kwamba uteuzi huo umeanza jana.

Katika hatua nyingine Sheikh Mataka alisema kumekuwa na matumizi yasiyo sahihi ya wadhifa wa Sheikh Mkuu kutumiwa na baadhi ya masheikh wa mikoa na wilaya.

Alisema kwa mujibu wa Bakwata wadhifa wa Sheikh Mkuu unamhusu Mufti wa Tanzania tu na kwamba chini yake ni Masheikh wa mikoa, wilaya na si vinginevyo.

Masheikh wa mikoa, wilaya na mitaa wanakumbushwa kutumia nyadhifa zao kama zilivyoainishwa katika Katiba ya Baraza kuu la Waislamu. Sheikh Lolila astaafu Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa Bakwata, Sheikh Suleiman Lolila amestaafu wadhifa huo kutokana na umri na afya yake.

Sheikh Lolila alisema kuwa licha ya kuomba kustaafu kwake atakuwa tayari kulisaidia baraza pindi watakapohitaji msaada wake wa kimawazo.

“Nimeomba kustaafu Bakwata hivyo naomba watu waelewe kuwa hali yangu inaendelea vizuri lakini watakapohitaji msaada wangu nipo tayari nitakuja kuwasikiliza na ninapoweza nitawasaidia,”alisema.

Hata hivyo baadhi ya viongozi wa baraza hilo wamempongeza kwa uamuzi huo na kuwataka wengine kuiga mfano wake kwa kuwa alikuwa kiongozi wa mfano.

“Nampongeza sana Katibu Mkuu kwa kuona kuwa jambo hili ni muhimu kwake kutokana na umri alionao na kama alivyosema kuhusu afya yake japo angependa kulihudumia baraza lakini ameona inatosha kuwaachia vijana maana wazee tuking’ang’ania watoto hawatasoma.”

“Tungependa uwe mfano wa kuigwa kwa kwa viongozi wa dini ambao wamekuwa wagumu kujiengua, kujiuaulu au kustaafu kwenye nafasi zao waige mfano wako, tumekuwa nae muda mrefu ndani ya baraza na tumefanya kazi kwa uaminifu na uadilifu kwa wakati wote bila kujali likizo.”

Sheikh Mataka alisema kuwa Sheikh Lolila alikuwa mtu ambaye pamoja na uzee alionao akiwa na kitu cha haraka hutembea kuanzia Bakwata hadi Ikulu hivyo baraza linaandaa utaratibu maalum wa kumuaga ili kutahmini kustaafu kwake.

Aidha nafasi hiyo itakaimiwa na Naibu Katibu Mkuu wa Bakwata, upande wa Utawala, Ustadhi Salim Abeid hadi itakapopata mtu.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo