CUF wasubiri JPM amtumbue Msajili


Fidelis Butahe

SIKU moja baada ya CUF kuanika jinsi Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ilivyobariki kambi inayoongozwa na Profesa Ibrahim Lipumba kuchukua Sh milioni 369.4 za ruzuku, chama hicho kimesema kinasubiri Rais John Magufuli atengue uteuzi wa Jaji Francis Mutungi.

Kimesema kutokana na Rais Magufuli kuwa mstari wa mbele kupambana na rushwa, ufisadi na ubadhirifu, kinaamini hatasita kumchukulia hatua Jaji Mutungi kwa madai kuwa amebariki ubadhirifu na utakatishaji wa fedha kinyume na sheria.

“Tunasubiri kuona kama atamtumbua au la au atampandisha cheo. Awali (Mutungi) alizuia ruzuku kutoka, iweje sasa aitoe wakati chama kina mgogoro? Tunajadiliana ikishindikana tutampeleka mahakamani, licha ya kuwa tayari tumemfungulia kesi na inaendelea,” alisema Nassor Ahmed Mazrui, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Zanzibar.

Juzi Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Chama hicho, Julius Mtatiro alisema ruzuku hiyo iliyokuwa imezuiwa na Ofisi ya Msajili imeanza kutoka na mnufaika ni Profesa Lipumba ambaye anatambuliwa na ofisi hiyo.

Alisema kitendo hicho kimefanywa na viongozi wanaomuunga mkono Profesa Lipumba, watendaji wa Serikali na maofisa wa benki iliyotoa fedha hizo.

Mtatiro alisema wanachama wanaomuunga mkono Profesa Lipumba walichukua fedha hizo kupitia akaunti ya CUF Temeke, kisha wakazihamishia kwenye akaunti binafsi tofauti, wakati fedha za ruzuku huwekwa kwenye akaunti kuu inayosimamiwa na Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad.

“Ni kudhihirisha namna gani Msajili anavyotumika. Yeye ndiye alileta mgogoro CUF kwa kuridhia Lipumba aendelee kuwa mwenyekiti. Oktoba 10 alisitisha ruzuku kutokana na mgogoro wa kiuongozi uliokikumba chama, ila bila chochote ameruhusu fedha kutoka,” alisema Mazrui.

“Fedha zimetoka kinyume na taratibu na sheria. sijui kwa kweli labda naye ana mgao wake.”

Alisema kutokana na hali hiyo, wanasubiri hatua za Rais Magufuli dhidi ya Msajili huyo na kusisitiza kuwa iwapo kiongozi mkuu wa nchi atasita kumtumbua Jaji Mutungi, atakuwa anadanganya Watanzania.

“Rais Magufuli anapigania haki na kutetea wanyonge na masikini. Katika hili ajitokeze na kumchukulia hatua Msajili. Kama anapigania haki ya wanyonge achukue hatua katika hili,” alisema.

Jana gazeti hili lilimtafuta Jaji Mutungi ambaye awali aliahidi kufuatwa ofisini kwake, ili kupata ufafanuzi wa suala hilo na mengine lakini badala ya kutoa ufafanuzi, alisema ana shughuli nyingi atafutwe siku nyingine.

Kuhusu kesi, Mazuri alisema licha ya kuwa kesi ya awali ipo mahakamani, chama hicho kitajadili kwa kina uamuzi huo na wajumbe wakikubaliana, watamfungulia kesi nyingine Msajili.

“Tutaitisha vikao vya Kamati Tendaji na Baraza Kuu la Uongozi, vikiamua tutamshtaki. Vikao hivyo vitafanyika siku za karibuni, si unajua hatuna ruzuku hivyo lazima tuchangishane, tutafute mahali mwafaka pa kufanyia,” alisisitiza.

Oktoba mwaka jana, Bodi ya Wadhamini CUF ilifungua kesi Mahakama Kuu. Katika kesi hiyo, Bodi inaiomba Mahakama itoe amri ya kubatilisha barua ya Msajili inayomtambua Profesa Lipumba kuwa mwenyekiti wa chama hicho.

Pia, wanaiomba Mahakama itoe amri ya kumzuia Msajili kufanya kazi nje ya mipaka yake ya kisheria katika utekelezaji wa majukumu yake na pia itoe amri ya kumzuia kuingilia masuala ya kiutawala ndani ya chama hicho.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo