Mbunge Lijualikali afungwa miezi 6


Peter Kimath, Morogoro

Peter Lijualikali
MAHAKAMA ya Wilaya ya Kilombero imemhukumu Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali (30), kifungo cha miezi sita kwa kufanya vurugu na kusababisha taharuki kwenye mkutano wa uchaguzi wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Mdogo wa Ifakara.

Mwendesha Mashitaka Inspekta wa Polisi, Dotto Ngimbwa awali alidai mahakamani hapo kuwa mshitakiwa namba moja (Peter) na mwenzake Stephano Mgata (35) walitenda kosa hilo Machi mosi, mwaka jana Kibaoni kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.

Ngimbwa alidai kuwa siku hiyo saa 4 asubuhi Kibaoni washitakiwa walifanya fujo na kusababisha uvunjifu wa amani katika eneo hilo. Washitakiwa walikana mashitaka na kesi kuanza kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili na upande wa mashitaka kuthibitisha tuhuma bila kuacha shaka.

Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya Kilombero, Timothy Lyon, alisema Mahakama iliwatia hatiani kwa kosa hilo na kwa kuwa mshitakiwa wa kwanza alikuwa na kesi tatu huko nyuma na kutiwa hatiani na kuhukumiwa, atafungwa miezi sita.

Lyon alitaja kesi za nyuma ambazo mbunge huyo alitiwa hatiani na kuhukumiwa kuwa ni kesi namba 338 ya mwaka 2014, kesi namba 220 ya mwaka 2014 na kesi namba 340 ya mwaka 2014.

Alisema Mahakama kwa kuona mshitakiwa ni mzoefu na kuona katika kesi zote alitiwa hatiani hivyo Mahakama iliona mtuhumiwa ana hatia na kustahili kutumikia kifungo cha miezi sita jela.

Hata hivyo, Mahakama hiyo ilimwona mshitakiwa wa pili Stepheno Mgata ilikuwa ni mara yake ya kwanza kutenda kosa, na hivyo kumhukumu kifungo cha nje cha miezi sita na ndani ya kipindi hicho hatatakiwa kutenda kosa lolote la jinai.

Katika hali isiyo ya kawaida Mahakama hiyo ilikuwa tulivu tofauti na kesi zilizopita ambapo wanachama wachache walijitokeza, licha ya kusambazwa kwa ujumbe wajitokeze kwa wingi siku ya hukumu.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo