Bara, Z’bar kuunda Kamati ya gesi, mafuta


Mwandishi Wetu

WIZARA ya Nishati na Madini kwa kushirikiana na  Wizara ya  Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira ya Zanzibar, zinatarajia kuunda Kamati maalumu kwa ajili ya  kuandaa mpango wa ushirikiano kati ya Tanzania Bara na  Zanzibar katika  sekta za gesi na mafuta.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo  alibainisha hayo katika kikao chake na  Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira Salama Aboud Talib  aliyeambatana na ujumbe wake.

Kikao  hicho kilihudhuriwa na watendaji kutoka  Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Maendeleo ya Petroli  Tanzania (TPDC),  Shirika la  Umeme Tanzania (Tanesco), Mamlaka ya Udhibiti  wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), Wakala wa Uagizaji  wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Shughuli za Mkondo wa Juu wa Mafuta (PURA).

Profesa Muhongo alisema lengo la kamati hiyo ni kujadili maeneo ya kushirikiana pamoja na kubadilishana uzoefu katika sekta za gesi na mafuta.

Alisema kamati hiyo itashirikisha wataalamu kutoka katika taasisi za Sheria, ardhi, kodi, gesi na mafuta  chini ya makatibu wakuu wa sekta husika kutoka Tanzania Bara na  Zanzibar.

Waziri Muhongo alisema uwepo wa kamati hiyo utachochea Zanzibar kuwa na taasisi kama TPDC na nyingine, hivyo kupelekea ukuaji wa sekta ya gesi na mafuta.

Alisisitiza kwamba Serikali ya  Tanzania Bara kupitia  Wizara ya Nishati na Madini ipo tayari kushirikiana na  Serikali ya  Zanzibar pamoja na kubadilishana uzoefu katika  masuala ya gesi na mafuta.

Profesa Muhongo alishauri  Serikali ya  Zanzibar kuandaa wataalam wa mafuta  na gesi  kwa kuwasomesha katika ngazi za diploma na shahada katika  Chuo Kikuu cha  Dar es Salaam (UDSM) na  Chuo cha Madini  Dodoma (MRI).

Akiongeza Serikali ipo tayari kutoa ufadhili kwa wanafunzi wa Zanzibar wanaofanya vizuri katika masomo ya  Sayansi kwa ajili ya kusomea shahada ya uzamili katika  vyuo vya  ndani na nje ya nchi.

Naye Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira Zanzibar, Salama Aboud Talib, alimshukuru Waziri Muhongo kwa utayari wa Wizara  ya Nishati na Madini  katika kushirikiana na Wizara yake kwenye shughuli za mafuta na gesi

Alisema kamati itakayoundwa itapelekea mambo kwenda kwa kasi na kuwa na data za pamoja zinazotokana na utafiti wa mafuta na gesi na kupanga Mikakati ya kuvutia wawekezaji kutoka nje ya nchi.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo