Jamhuri yatakiwa kubadili hati ya mashitaka


Grace Gurisha

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu,Dar es Salaam imetoa siku mbili kwa upande wa Jamhuri kubadilisha hati ya mashitaka  ya mauaji dhidi ya mke wa bilionea Erasto Msuya (marehemu), Miriam Msuya (41), anayetuhumiwa kumwua dada wa Msuya, Aneth, baada ya kubainika kuwa hati hiyo ina kasoro.

Pia Mahakama hiyo imeitaka mamlaka husika itoe fomu ya matibabu (PF3) kwa Miriamu na mshitakiwa mwingine, Revocatus Muyela (40) wakatibiwe, baada ya kuieleza Mahakama kuwa waliteswa na polisi ili wakiri kutenda kosa hilo.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi, Godfrey Mwambapa wa Mahakama hiyo, akisema baada ya kupitia hati hiyo, alibaini kasoro mbili za kisheria, kuwa hati hiyo haioneshi mtu mmoja kusababisha kifo cha mtu mmoja.

Kasoro ya pili, Mwambapa alisema mtu aliyesababisha kifo haonekani kama ana nia ovu, kwa hiyo washitakiwa hawaonekani kama walitenda kosa hilo, hivyo Mahakama inaona hati hiyo ni mbovu na si sahihi.

“Siwezi kusema hati hii ni sahihi kwa sababu tu imepokewa na Mahakama, kwa hiyo kasoro hii inatakiwa irekebishwe ndani ya siku mbili. Hatua hiyo inatokana na Mahakama kuwa na mamlaka ya kusahihisha hati ya mashitaka kabla ya kwenda Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na pia inaweza kuamuru hati ibadilishwe,” alisema Mwambapa

Katika suala la kuteswa kwa washitakiwa, Hakimu Mwambapa alisema Mahakama inaona suala hilo ni la msingi, hivyo hatua za makusudi zinaweza kuchukuliwa yanapotokea malalamiko kama hayo, hivyo alikubaliana na hoja za wakili wa utetezi Peter Kibatala, kuwa Mahakama haizuiwi kuamuru mamlaka husika kuwapa PF3.

Alisema hatua hiyo inatokana na kwamba Mahakama haina utaalamu kuhusu masuala ya kiafya, kwa hiyo yanapotokea lazima yafikishwe kwenye mamlaka husika hivyo inatakiwa iwape fomu ili wakapewe matibabu, lakini haina maana Mahakama inahitaji matokeo hayo.

Alisema hati ibadilishwe na ipelekwe mahakamani na kesi iliahirishwa hadi Januari 11   Jamhuri itakapokuwa imerekebisha kasoro zilizopo.

Hatua hiyo ilifikiwa na Mahakama hiyo, baada ya Kibatala kuwasilisha maombi hayo kwa Hakimu Mkazi Magreth Bankika kuwa hati ya mashitaka ina kasoro na kuomba ifutwe pia akidai kuwa wateja wake waliteswa na polisi.

Mbali na Miriam, mshitakiwa mwingine ni mfanyabiashara wa Arusha, Revocatus Muyela (40), ambapo Kibatala alidai pia kuwa washitakiwa hao waliteswa na askari kabla ya kuchukuliwa maelezo ili wakiri kuhusika na mauaji hayo.

Akijibu hoja hizo, Wakili wa Serikali, Diana Lukondo alidai kuwa hati hiyo ya mashitaka iko sahihi kwa kuwa ina sababu zote za kuitwa hati ya mashitaka, hivyo hoja za Kibatala hazina mashiko.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo