Ajali ya mashua yaua watu 12 bahari ya Hindi


Mariam Cyprian, Tanga

WATU 12 waliokuwa wakisafiri na mashua iliyokuwa ikitoka Tanga kwenda Pemba wamekufa maji na miili yao kuopolewa baada ya chombo hicho kukumbwa na dhoruba iliyotokana na upepo mkali wa Kaskazi.

Abiria 34 waliokolewa na wavuvi waliokuwa wakivua kwenye bahari ya Hindi eneo la Jambe jirani na pwani ya mkoa wa Tanga.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana na kuthibishiwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba, mashua hiyo iliyokuwa ikiendeshwa na nahodha Badru Said ilipigwa na dhoruba saa mbili usiku wa kuamkia jana.

Abiria walionusurika walisema chombo hicho kiling'oa nanga kwenye bandari ya Sahare jijini hapa juzi saa moja usiku kwenda Wete, Pemba ikiwa na abiria 52 na shehena ya mizigo ikiwamo mifuko ya mchele, pumba, viazi, maharage na masanduku ya bia.

Walisema baada ya kufika eneo la Jambe mashua hiyo ilipigwa na dhoruba kwa nyuma na kupoteza mwelekeo na kwa kuwa kulikuwa na upepo mkali, abiria walizama baharini.

Mkubwa Yussuph Hassan (55) alisema kuzama kwa mashua hiyo, kulitokana na kutoboka kwa chini na maji kuingia kwa kasi na ndani ya dakika 15 yalijaa na kusababisha kila kilichokuwamo kulowa.

"Kitendo hicho cha kupigwa na dhoruba kilikuwa ni cha muda na chombo kujaa maji kilikuwa ni cha muda mfupi sana hivyo hatukuwapigia simu jamaa zetu wa Pemba na Tanga kwa sababu simu zilijaa maji na kushindwa kufanya kazi," alisema Mkubwa mzaliwa wa Pemba na mkazi wa mtaa wa Nguvumali jijini hapa.

Mussa Isah Mohamed (37) wa Kengeja, Pemba aliyekuwa na mtoto wa kaka yake, alisema yeye alinusurika baada ya kuogelea hadi kufikia chombo cha wavuvi.

"Nasikitika mtoto wa kaka niliyekuwa nakwenda naye Pemba amekufa, ilifika mahali nilishindwa kumwokoa nikawa sina jinsi zaidi ya kumuaga na kumwambia ‘tangulia ndugu yangu hakuna namna’," alisema Mussa huku akitokwa machozi.

Aidha wavuvi waliofanya uokoaji walisema baada ya kubaini kuwa mashua hiyo imezama, walipiga mbizi na kuibua miili ya waliokufa na wengine waliokuwa hai.

"Tunashukuru Mungu alitupa nguvu ya kupiga mbizi kwenye maji marefu ya Jambe, tuliokoa abiria 34 na miili ya tuliokuta wameshakufa maji," alisema Mbwana Hamis Mbwana.

Kamanda Wakulyamba alisema abira 12 akiwamo nahodha wa mashua hiyo, Badru walikufa maji huku wengine 34 wakiokolewa na kufikishwa hospitali ya Bombo kwa matibabu.

Alisema mashua hiyo iliyotoka jijini hapa kutoka bandari bubu ya Sahare, ilikuwa imebeba magunia 30 ya pumba, mchele magunia 10, maharage magunia 15 na masanduku ya bia.

Kamanda alisema majina ya waliokufa na majeruhi atayataja baada ya ndugu zao kuwatambua.

Ofisa wa Mamkala ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) Mkoa wa Tanga, Dk Walukani Luhamba alisema ajali hiyo ni matokeo ya manahodha kupuuza maelekezo ambayo yamekuwa yakitolewa, kuhusu kufuata sheria na taratibu za usafiri majini.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo