Wakazi hao
wameilalamikia Serikali kwamba haikuwashirikisha katika hatua hiyo inayolenga
kupisha mradi wa uchimbaji madini ya graphite unaoendeshwa na Kampuni ya
TanGraphite, chini ya kampuni tanzu ya Kibaran Resources ya nchini Australia.
Wakazi hao waliliambia
gazeti hili kuwa tangu mradi huo uanze mwaka 2012 na wao kutakiwa kuhama
maeneo yao hayo ya asili, kumeibuka sintofahamu kubwa, huku mambo mengi yakiamuliwa
bila wao kupewa fursa ya kushiriki. Walisema kumekuwa na matumizi ya nguvu hasa
kwa wananchi wanaonekana kuhoji. Watu wanatishwa na wengine wanakamatwa na
polisi, jambo ambalo linawafanya wakose amani, alisema mmoja wa wakazi hao
ambaye hakutaka kutajwa kwa hofu ya kukamatwa kama ilivyotokea kwa wenzake
kadhaa.
“Awali tulipopewa
taarifa ya kuhama ili tupishe mradi, tulihoji mambo kadhaa, lakini inaonekana
kwamba Kampuni hii ya TanGraphite ilishaanza kazi, hivyo wakatupuuza. Kuanzia
viongozi wa kijiji hadi mkoa hakuna aliyetusikiliza,” alisema.
Mwanakijiji huyo
aliyeambatana na wenzake kadhaa kwenye ofisi za gazetili kuleta malalamiko
hayo alisema, kimsingi wakazi hao hawapingi mradi, ila wanataka kushirikishwa
ili wajue hatima yao. “Kampuni imeshaanza kazi na wanatutaka tuhame, lakini
hawatwambii twende wapi na tunaenda vipi. Sasa haya ndiyo mambo tunayosema kuwa
hayako vizuri tunahitaji kushirikishwa tujue hatima yetu,” alisema.
Mkazi huyo alibainisha
kuwa tangu mradi huo uanze hawakuambiwa chochote, lakini baada ya kulalamika
Kampuni ya Mtei ilifika kijiji hapo kwa ajili ya kufanya tathmini ya makazi
yao, lakini hata hivyo bado kuna usiri unagubika.
Kauli
ya Serikali
Alipotakiwa kuzungumza
suala hilo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi
alitaka aulizwe Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
Waziri Muhongo alisema
haamini kama wananchi hao wanaonewa kwani alituma watu mara nyingi ili waweze
kuwasaidia kumaliza mgogoro huo.
“Ngoja nikwambie waambie
hao wananchi washike Msahafu na Biblia waseme kama hawajawahi kushirikishwa na
Serikali ya Mtaa na kusaidiwa katika suala hilo,”alisema.
Alisema vitengo
mbalimbali Serikaliani ikiwamo, Kamishna wa Madini, mkuu wa wilaya na mkuu wa
mkoa wamekuwa mstari wa mbele kuwasaidia wananchi kwa namna tofauti.
Waziri Muhongo akamtaka
mwandishi wa habari hii kuwasiliana na mkuu wa wilaya ya Ulanga kuzungumzia
suala hilo kwa kuwa tayari ofisi yake ilishatoa maelekezo kwake kushughulikia
suala hilo.
DC
anena
Mkuu wa Wilaya ya
Ulanga, Jacob Kasemma alisema katika jitihada za kutatua mgogoro huo, Serikali
kwa kushirikiana na Kampuni ya TanzGraphite waliamua kujenga ofisi ambayo itasikiliza
malalamiko na maoni ya wananchi hao lakini baadhi yao waliivamia na kuivunja.
“Kule ni kijijini,
tuliamua kujenga ofisi maalumu kusikiliza kero, malalamiko na maoni na
madukuduku ya wananchi kwa lengo zuri kabisa ili kuondoa tofauti zilizopo,
lakini baadhi ya wananchi walivamia ofisi hiyo na kuivunjavunja, huku
wakitishia usalama wa maofisa waliowekwa pale. Kumbe unaweza kuona kuwa suala
hilo lina changamoto kubwa,” alisema.
Akizungumzia madai ya wananchi
hao kwamab wamekuwa wakikamatwa na polisi, mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa
suala hilo halipo isipokuwa wananchi wanachojaribu kufanya ni kuihadaa jamii
kuhusu jambo hilo.
“Kuna wananchi walivamia
sehemu vilipowekwa vifaa vya kampuni ya TanzGraphite kwa lengo la kufanya
uharibifu. Sasa suala la uharibifu wa mali ni jinai, hivyo Polisi lazima
wachukue hatua. Jambo mbaya sana linalofanywa na hao watu wachache ni kwamba
waliwatumia wanafunzi, na baada ya hapo walizusha habari kwamba Polisi imepiga
mabomu wanafunzi,” alisema. Alibainisha kuwa anafahamu uwepo wa watu wachache
kupinga mradi huo, lakini bado anafanya juhudi za kukutana nao ili kujua msingi
wa madai yao.
Mkuu
wa Wilaya wa zamani
Awali, aliyekuwa mkuu wa
wilaya hiyo kabla ya Kasemma Christine Mndeme alisema madai ya wananchi hao
hayana msingi kwa kuwa hayaeleweki.
“Mradi huo ulipitia
hatua zote. Tulianza na vikao vya kijiji, lakini mkutano wa kijiji watu hawakuhudhuria.
Binafsi kama Mkuu wa Wilaya niliwaita wananchi hao mmoja mmoja niwasikilize,
lakini hawakufika. Baadaye wakazusha kwamba nimewaita ili niwahonge pesa na
wengine wakasema nimewaita ili niwakamate, hivyo hadi naondoka tumeshindwa
kujua hoja yao ni nini,’ alisema.
Mwekezaji
anasemaje?
Mkurugenzi Mtendani wa
Kampuni ya TanGraphite, Grant Pierce alisema hakuna sababu yoyote ya wananchi hao
kuwa na wasiwasi juu ya mradi huo kwa kuwa mchakato wake bado unaendelea.
“Ni kweli hadi sasa
hakuna mwananchi anayejua atahamia wapi kwa sababu kwa kushirikiana na
Serikali ya Mkoa, Wilaya na Serikali ya kijiji tupo katika mchakato wa kutafuta
maeneo ambayo tutawajengea makazi wananchi hao. Tumeunda kamati yenye
wawakilishi wanne kutoka vitongoji sita vya kijiji hicho kwa ajili ya kufanya
shughuli hiyo,” alisema.
Mradi
ukoje?
Mradi wa uchimbaji madini ya graphite, ulianza mwaka
2012 kwa kampuni ya TanzGraphite kuanza kufanya utafiti. Mradi huo utadumu kwa
miaka 27 na utahusisha vitongoji vitatu katika kijiji cha Epanko. Wakati wa
kitongoji cha Epanko A na Kazimoto watahamishwa kupisha mradi huo. Pia nusu ya
wakazi wa Kitongoji cha Itatira watatakiwa kuhama. Mradi huo hautagusa
vitongoji vingine viashughuli za uchumbaji wa madini hayo huku nusu ya
kitongoji cha Itatira ikiguswa. Vitongoji vingine vitatu vya Epanko B Mbera na
Lurina havitaguswa kabisa.
0 comments:
Post a Comment