KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imesema Tanzania
inapoteza kiasi kikubwa cha mapato kutokana na kushindwa kuhifadhi mafuta
yanayoingizwa nchini hivyo kusababisha waagizaji kuhifadhi kwenye maghala
binafsi.
Kauli hiyo ilitolewa juzi na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dotto
Biteko alipokuwa akifanya majumuisho ya vikao vya kamati hiyo kwa waandishi
wa habari.
“Kamati inaisisitiza Serikali kujenga mahali maalumu pa kuhifadhi
mafuta yanayopakuliwa kutoka kwenye meli, kabla ya kwenda kwa wanunuzi ili
kuisaidia kuwa na uhakika wa kiasi cha mafuta yaliyoagizwa nchini,” alisema.
Aliongeza kwamba hilo pia litasaidia kupata uhakika wa kodi
stahiki za Serikali kujua kama zimelipwa, usalama pamoja na kuondoa mianya ya
wizi inayoweza kujitokeza.
Biteko ambaye pia ni Mbunge wa Bukombe (CCM) alisema mafuta
yanapoagizwa yanaposhuka bandarini yanapaswa kufika katika kituo kimoja
ambacho, wafanyabiashara wote wa nishati hiyo watachukua.
Alisema hatua hiyo imekuwa ikisababisha mianya ya wizi huku
akiitaka Serikali kuhakikisha inakuwa na sehemu moja ya kuhifadhia mafuta
kabla hayajasambazwa.
“Kamati yetu imeafanya kazi na wadau mbalimbali wakiwemo Mamlaka
ya Bandari Tanzania (TPA), tulipowauliza kuhusu utaratibu wa usambazaji
mafuta, wamekiri ni Tanzania pekee ambayo unaweza kuyaingiza nchini na kila
mfanyabiashara akaweka kwenye ghala lake, nchi nyingine yanawekwa kwenye ghala
la pamoja la Serikali kwanza kabla ya kwenda kwa wafanyabiashara binafsi,”
alisema.
Alifafanua kuwa, “kwenye mnyororo wa mafuta, TPA ndiye anahifadhi
mafuta, lakini anahifadhi mafuta kidogo sana na kila muagizaji anahifadhi
kwenye ghala lake, wakati umefika Serikali itengeneze eneo malumu la
kuyahifadhi yakitoka kwenye meli”.
Alisema hali hiyo itasaidia Serikali kuwa na uhakika wa kiasi
mafuta yaliyoagizwa nchini, itakuwa na uhakika wa kulipwa na kodi stahiki za
Serikali, usalama wa mafuta na kuondoa mianya ya wizi mdogo mdogo unaofanyika.
Pia kamati hiyo imeiagiza Serikali kupeleka majibu ya kutosha kwa
kamati hiyo kuhusu sakata zima la uagizaji mafuta mabovu na upungufu wa mafuta
ya taa ili jambo hilo lisijitokeze tena nchini.
Alisema wameiomba Wakala wa Uagizaji Mafuta wa Pamoja (PPA )
watoe maelezo ya kutosha kwa nini kulitokea changamoto ya upungufu wa mafuta ya
taa nchini na hatua zilizochukuliwa.
0 comments:
Post a Comment