Viongozi serikalini wafugaji wahusishwa mapigano


Sharifa Marira, Rufiji

Mohamed Mchengerwa
MBUNGE wa Rufiji, Mohamed Mchengerwa (CCM), amesema viongozi wengi serikalini ni wafugaji ndiyo maana wanashindwa kushughulikia migogoro ya wakulima na wafugaji, ambayo imekuwa ikisababisha madhara makubwa kwa wananchi.

Mchengerwa alitoa kauli hiyo jana alipozungumza na wananchi wa kijiji cha Mgomba Kati, walioeleza jinsi wafugaji wanavyoingiza mifugo yao kwenye mashamba ya wananchi, wakiwa hawajavuna.

"Wafugaji wanatuumiza, lakini haya yote ni kwa sababu viongozi wengi ni wafugaji, hivyo wanashindwa kuingilia kati suala hili, badala yake wanaacha wananchi wauane kila kukicha, utafika wakati tutashindwa kuvumilia haya, tunakufa njaa na umasikini kwa sababu ya watu.

"Yametokea matukio makubwa ya kuuawa wananchi wawili kwenye kijiji cha Kilimani mwezi jana, lakini sikuona kiongozi wa Serikali aliyetoa tamko au hata kufika eneo la tukio, vivyo hivyo hata kwa yule mwananchi wa Morogoro aliyechomwa mkuki kinywani ukatokea shingoni, viongozi wametulia tu," alisema.

Alisema si Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba, Naibu wake, William ole Nasha wala makatibu wakuu wao, waliofika maeneo yaliyoathirika au hata kutolea   makatazo dhidi ya mambo hayo na kwamba ndiyo matunda ya viongozi wengi wafugaji hivyo kushindwa kutafuta suluhisho la kudumu.

Alisema kuwapo mifugo Rufiji kulitokana na rushwa ya viongozi waliokuwa madarakani miaka ya 2005, ambao walitoa mifugo kwenye bonde moja ili lisiharibike na kupeleka  bonde lingine ili kuua wananchi wa maeneo hayo.

"Mifugo hapa kwetu ilikuja mwaka 2005, ilihamishwa kutoka bonde la Ihefu, Iringa, kwa kuwa lilikuwa likiharibika, lakini cha kushangaza ikaletwa bonde la Rufiji ili liharibike nasi wananchi tupate shida na ndicho kinachotokea leo hii," alisema Mchengerwa.

Alieleza kuwa alichaguliwa na wananchi kuwawakilisha vema na kutetea maslahi yao na ndicho anachokifanya na hatarudi nyuma katika kudai haki na maendeleo ya Rufiji, kwani imekuwa nyuma kwa miaka mingi kutokana na kukosa wawakilishi wenye nia ya dhati ya kuwasaidia.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo