‘Mahausigeli’ wawa miiba kwa ndoa Dar


Celina Mathew

WASICHANA wa kazi wametajwa kuwa chanzo cha kuvurugika kwa ndoa nyingi Dar es Salaam, kutokana na uhusiano zaidi ya kazi za nyumbani wanaokuwa nao na mabosi wao.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi katika mahojiano maalumu jana, Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Polisi, Dawati la Jinsia wa Wilaya ya Kinondoni, Inspekta Prisca Komba alisema visa vya wasichana hao vimekuwa vikiripotiwa Polisi.

Inspekta Prisca alisema kwa upande wa mabosi wa kiume, wasichana hao wamekuwa wakishirikiana nao ngono mara nyingi baada ya mabosi kutumia kilevi, lakini wakati mwingine wakibakwa.

"Unakuta baba anakunywa pombe na kulewa sana na anaporudi nyumbani kama mama hayupo, anaamua ‘kutembea’ na mfanyakazi wake wa ndani, jambo linalofanya kina mama kuja kushitaki kwa kuwa baada ya hapo wengine hufukuza wake zao na kuwapiga wanapowahoji," alisema.

Kwa upande wa wanaume, Inspekta Prisca alisema baadhi wamekuwa wakilalamika kuwa wasichana wa kazi wamegeuka makuwadi wa wake zao, jambo wanaloona kuwa wananyanyasika.

Alitoa mfano wa mwaka jana, ambao wanaume 25 walifungua kesi za kudhalilishwa na wake zao kwa kunyimwa unyumba hali iliyowasababishia kuchepuka.

"Unakuta mwanamke anamwambia mumewe kwamba ana maumbile madogo wakati walishazaa watoto wawili na kuna baadhi ya wanawake walilalamikiwa kuhodhi mali za waume zao na kuzipeleka kwa ndugu zao ambao hawahusiki nazo," alisema.

Alisema wanawake watano walihodhi mali na wengine wawili walilalamikiwa kuwa na nyumba ndogo.

Akizungumza kisa asichokisahau katika Dawati hilo, Inspekta Prisca alisema ni cha binti Yusta Lucas (20), mwenyeji wa Tabora ambaye alifika Dar es Salaam kufanya kazi za ndani na kufanyiwa ukatili wa kung’atwa meno na bosi wake.

Alisema kesi ya binti huyo ilimalizika Novemba mwaka jana, ambapo mhusika alihukumiwa kifungo cha maaka miwili na faini ya Sh milioni 2 na kufungwa kifungo cha nje.

Kwa mujibu wa Inspekta Prisca, asilimia tano ya wanawake wamekuwa wakilalamika kunyimwa unyumba na waume zao, jambo linalowafanya kutoka nje ya ndoa na baadhi ya wanaume pia hukataliwa na wake zao.

Alisema kwa kiasi kikubwa, hali hiyo husababishwa na kukua na kubadilika kwa sayansi na teknolojia, ambayo baadhi yao wamekuwa wakijidanganya nayo.

Wakwe

Inspekta Prisca alisema kunapokuwa na kesi za visa vya mama wakwe na mawifi, wamekuwa wakiwaita wakwe na kuwaeleza kuwa wao walishafanikiwa kwenye ndoa zao zilizodumu, hivyo wawaache watoto wao nao wafaidi ndoa zao badala ya kuziingilia.

"Wapo kinamama wengi wanaopigania sana watoto wao wa kike walioolewa hadi ndoa zao zinakosa nguvu,” alisema.

Alitaja pia changamoto ya wanaume walioacha wake zao kuamua kubaki na watoto, ili wanyanyase watalaka wao, wakati sheria inasema kila mtoto anatakiwa kukaa siku 15 kwa mama na nyingine 15 kwa baba.

Akizungumzia takwimu za mwaka jana kuanzia Januari hadi Desemba, Inspekta Komba alisema kesi zilizoripotiwa za kubaka zilikuwa 62, kulawiti 19, shambulio la aibu 12, kutorosha watoto 23 na kutelekeza familia 32.

Kesi 12 za kufanya mapenzi na wanafunzi ziliripotiwa, kuwapa mimba wanafunzi 13, shambulio la kimwili 33, kujeruhi tisa, ukatili wa watoto moja, kutorosha wanafunzi 12, kunajisi moja na kujaribu kubaka tatu.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo