Tanzania yaingizwa mkakati wa kiuchumi China


Mwandishi Wetu

Samia Suluhu
TANZANIA imechaguliwa kuwa miongoni mwa nchi saba zilizoingizwa katika Mpango wa Ukanda wa Kimkakati wa Kiuchumi wa China.

Mpango huo ulibuniwa na Serikali ya China kwa dhamira ya kukutanisha jumuiya za wafanyabiashara za Mashariki mwa Asia, Mashariki ya Kati, Ulaya na Afrika, kubadilishana mawazo kuhusu kuwezesha biashara kuchangia kwenye uchumi wa mataifa yao.

Nchi zingine zilizochaguliwa kuingizwa kwenye mpango huo ni Malaysia, Sri Lanka, Nepal, Bangladesh, Pakistan na Thailand.

Taarifa ya Ofisi ya Makamu wa Rais iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana, ilieleza kuwa nafasi hiyo ya Tanzania, imepatikana baada ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan kufanya mazungumzo na mfanyabiashara wa madini na vito kutoka China, Dk Hellen Lau.

Makamu wa Rais, ambaye pia ni mjumbe wa jopo la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), la kumwezesha mwanamke kiuchumi, akiwakilisha nchi za Ukanda wa Kusini na Mashariki mwa Afrika, alikutana na Dk Hellen Septemba mwaka jana kwenye mkutano wa Guangdong, China.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa katika mkutano huo, Makamu wa Rais alimwomba Dk Hellen aisaidie Tanzania kuwasilisha maombi ya kuwa kwenye mpango huo na yalikubaliwa na kupata uanachama kwenye mpango huo mkubwa maarufu kama ‘China One Belt, One Road’.

Kutokana na uteuzi huo, Makamu wa Rais alikutana na watendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Chama cha Wafanyabiashara wenye Viwanda na Biashara (TCCIA) na Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI), kuwaeleza kuhusu muhimu wa Tanzania kuingizwa kwenye mpango huo.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa Samia alisema kwenye mpango huo kila nchi mwanachama imepewa ofisi kwenye jengo la 21st Century Maritime Silk Road Expo, bila kulipia kwa miaka mitatu, ili ioneshe na kutangaza bidhaa zake.

Samia aliwaagiza watendaji wa sekta binafsi wajipange na kuweka mikakati ya namna ya kunufaika na mpango huo haraka iwezekanavyo.

Alisema Tanzania pia itanufaika na fedha za mfuko kwa ajili ya maendeleo ya miundombinu, ambazo zinatolewa kwa nchi zilizojiunga na mpango huo.

Mwenyekiti wa TPSF, Godfrey Simbeye na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Wenye Viwanda na Wakulima Zanzibar, Taufik Turki walimwahidi Makamu wa Rais kutumia fursa hiyo ipasavyo kukuza biashara kati ya Tanzania na wanachama wa mpango huo.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo