Mchungaji alia ukata kanisani


*Adai ‘umebaka’ mpaka mfuko wake, ashindia uji
*Amwambia mwanawe hicho ni kipimo cha imani

Leonce Zimbandu

WIKI moja baada ya Rais John Magufuli kusema fedha zitapotea mpaka makanisani, Mchungaji wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) Viwege, Fulgency Bunduki amesimulia ukata ulioingia kanisani akisema ‘umebaka’ mfuko wake.

Jumapili ya kwanza ya mwaka huu, Rais Magufuli akiwa kwenye Kanisa la Bikira Maria Mama Mwenye Huruma wilayani Bukoba mkoani Kagera, aliwataka viongozi wa dini wamvumilie, kwa kuwa fedha zitaendelea kupotea hata kwenye nyumba hizo za ibada.

Rais Magufuli alisema zamani kulikuwa na fedha za hovyo hovyo, lakini sasa anachotaka ni kila mtu aendelee kula anachostahili, huku akiwataka Watanzania kufanya kazi kwa bidii kama maandiko matakatifu yanavyoelekeza kuwa asiyefanya kazi na asile, badala ya kulalamika kuwa fedha zimepotea.

Kwa kawaida vyanzo vikuu vya mapato kwenye nyumba hizo za ibada kwa maana ya makanisa na misikiti huwa ni sadaka zitolewazo na waumini.

Ukata

Akizungumza juzi kwenye ibada ya kuaga mwili wa mjumbe wa shina la CCM la Majengo Mapya, Kwa Mhaya, Kivule wilayani Ilala, Dar es Salaam, Mchungaji Bunduki alisema maisha yamekuwa ‘pasua kichwa’ si kwa wananchi pekee, bali hata kwa wachungaji, akiwamo yeye ambaye mfuko wake ‘umebakwa’ na ukata.

Akielezea visa vinavyoambatana na ukata, Mchungaji Bunduki alitoa mfano wa mwaka jana, siku aliyolazimika kunywa uji na familia yake mchana, ambapo mtoto wake wa kike aliuliza sababu za kunywa uji mchana na kuhoji kama baba yake ‘amefulia (amefilisika)’.

“Nilimjibu kuwa si kufulia bali njaa imebaka hata mifuko yangu, hivyo tuvumilie Mungu atatusaidia kusonga mbele,” alisema huku mamia ya waombelezaji wakivunja mbavu kwa kicheko.

Imani

Mchungaji Bunduki alisema kwa hakika hakuna binadamu aliyezaliwa na mwanamke atakayekwepa kifo, hivyo vikwazo vinavyotokea kwenye maisha sasa, ni matokeo ya kujiimarisha kiimani.

Alisema kutokana na hali mbaya ya maisha, baadhi ya Wakristo na Waislamu wamekuwa wakitoa visingizio vya kubanwa na kazi, kiasi cha kukosa muda wa kuhudhuria ibada makanisani au misikitini.

“Hii ni hatari mpaka kifo kinapotokea ndipo wachungaji au maimamu waonekane bora? Bora kusimamia usemi unaosema heri kuswali kabla hujaswaliwa,” aliwaasa waombolezaji.

Kukimbiwa

Baada ya Mchungaji Bunduki kumaliza kutoa mahubiri hayo, Mchungaji mwenyeji wa Kanisa hilo, Charles Mazengo aliasa waumini wa dini zote kuendelea kumwomba Mungu kwenye nyumba za ibada.

Alisema watu wamekuwa wasanii, kwani wanapoulizwa kuhusu Kanisa wanaloabudu, wamekuwa wakielekeza kwa vidole “ni pale”, lakini hata siku moja hawajawahi kufika kwenye Kanisa husika.

Mwenyeki wa Serikali ya Mtaa, Thomas Nyanduli aliwataka wakazi wa Majengo Mapya kuanzisha Mfuko wa Kufa na Kuzikana kwa vile hakuna ajuaye siku yake.

“Leo tumekusanyika hapa na kushikana mashati kwa ajili ya michango, lakini kama Mfuko ungekuwapo nguvu isingetumika, hivyo ni busara kujiwekea akiba,” alisema.

Uchunguzi wa gazeti hili kwa waumini wa makanisa mbalimbali, umeonesha kuwa baadhi ya yameanza kukusanya sadaka pungufu siku za ibada, ikilinganishwa na miaka kadhaa iliyopita.

Muumini wa moja ya makanisa ya Kimara, alilieleza gazeti hili kuwa kila wiki kwenye Kanisa analoabudu, walikuwa wakisomewa sadaka za hadi Sh milioni 20, lakini sasa kufikisha jumla kuu ya Sh milioni 10 ni nadra.

Mwingine wa Kanisa lililoko Hananasif, alidai kuwa Desemba mwaka jana kulijitokeza dalili za kupungua kwa sadaka na waumini, ingawa hakuwa na uhakika kama hali hiyo ilitokana na ukata unaozungumzwa.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo