Jalada lakwamisha kesi ya ‘Mpemba’


Grace Gurisha

UPANDE wa Serikali katika kesi ya Yusuf Yusuf ‘Mpemba’ (34) umeiambia Mahakama kuwa upelelezi umekamilika na jalada la kesi liko kwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda ya Dar es Salaam kwa uchunguzi zaidi.

Awali, Jamhuri uliiambia Mahakama hiyo juzi kuwa jalada hilo liko kwa Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Siro analifanyia kazi ili liende ngazi zingine kwa hatua zaidi.

Mkuu huyo akishamaliza kulifanyia kazi atalipeleka kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Biswalo Mganga kwa hatua zaidi za kulitolea uamuzi atakaoona unafaa katika kesi hiyo ili iendelee.

Awali, Wakili wa Serikali, Patrick Mwita alimwambia Hakimu Mkazi Mwandamizi Thomas Simba, kuwa mara ya mwisho Mahakama iliwataka watoe maelezo ya lilikofikia jalada katika upelelezi.

“Licha ya kwamba upelelezi umekamilika, lakini bado jalada liko kwa Kamanda Siro analifanyia kazi kabla ya kulipeleka kwa DPP kwa hatua nyingine,” alidai Mwita. Kesi hiyo iliahirishwa hadi Januari 23 itakapotajwa.

Mbali na Mpemba ambaye ni mkazi wa Tegeta, washitakiwa wengine ni Charles Mrutu (37) wa Mlimba, Morogoro, Benedict Kungwa (40) wa Mbagala Chamazi, Jumanne Chima (30) wa Mbezi, Ahmed Nyagongo (33) dereva na Pius Kulagwa (46).

Washitakiwa hao wanadaiwa kujihusisha na mtandao wa ujangili na biashara ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh milioni 785.6.

Ilidaiwa kuwa katika tarehe zisizofahamika kati ya Januari 2014 na Oktoba, mwaka jana wakiwa Dar es Salaam, Tanga, Iringa na Mtwara, walikusanya na kuuza vipande 50 vya meno ya tembo vyenye thamani ya dola 180,000 sawa na Sh milioni 392.8 mali ya Serikali bila kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Aliendelea kudai kuwa katika mashitaka ya pili, Oktoba 26 mwaka jana washitakiwa wakiwa Mbagala Zakhem, Temeke walikutwa na vipande 10 vyenye uzito wa kilo 13.85 na thamani ya dola 30,000 sawa na Sh milioni 65.4.

Ilidaiwa kuwa katika mashitaka ya tatu, Oktoba 27 mwaka jana washitakiwa wakiwa Tabata Kisukuru, walikutwa na vipande vinne vyenye uzito wa kilo 11.1 na thamani ya dola 15,000 sawa na Sh milioni 32.7.

Pia Oktoba 29 mwaka jana walikutwa na viapande 36 vya thamani ya Sh milioni 294.6.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo