Suleiman Msuya
RAIS John Magufuli amenusa ufisadi wa zaidi ya Sh bilioni
700 kwenye miradi ya undelezaji wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu
Nyerere (JNIA), na Uwanja wa Ndege wa Mwanza.
Aidha, amewatolea uvivu wahandisi nchini kwa kuwaambia
kuwa iwapo Tanzania haitafikia uchumi wa kati na wa viwanda wao ndio
watalaumiwa.
Rais Magufuli alisema hayo jana wakati akizungumza na
wahandisi zaidi ya 2,500 wanaoshiriki Mkutano Mkuu wa 14 jijini Dar es Salaam.
Alisema baada ya kupitia miradi hiyo, aliingiwa shaka na
gharama za ujenzi huo kuwa kubwa kuliko hali halisi jambo ambalo linamsukuma
kufikiria kufanya uchunguzi.
Rais Magufuli alisema matengezo ya upanuzi wa uwanja wa
JNIA umegharimu zaidi ya Sh bilioni 600 gharama ambazo anazitilia shaka huku
uwanja wa Mwanza ukigharimu zaidi ya Sh bilioni 100.
Alisema hofu iliongezeka baada ya Serikali kufanya
tathmini ya uboreshaji wa viwanja vingine vinane nchini ambavyo vimetengewa Sh
bilioni 100 huku maboresho kwa kila kiwanja yakigharimu zaidi ya Sh bilioni 11
kila kimoja.
“Haiwezekani viwanja vinane tuvifanyie maboresho kwa Sh
bilioni 100 halafu viwanja viwili vigharimu zaidi Sh bilioni 700 nafikiria
kufanyia uchunguzi katika viwanja hivyo,” alisema.
Alisema jambo la kusikitisha ni kuona kuwa gharama
zimetumika kufanyia upanuzi wa njia za kurukia na majengo ya kusubiria abiria
hivyo kuwataka wahandisi wajitafakari.
Rais Magufuli alisema kwa sasa wanakamilisha maboresho
katika kiwanja cha Dodoma kwa zaidi ya Sh bilioni 11 na wanaendelea na viwanja
vya Songea, Sumbawanga, Musoma, Tabora na vingine, ili kuboresha huduma ya
usafiri wa ndege nchini.
Kauli hiyo ya Magufuli imekuja baada ya kuzungumzia
uamuzi wa Serikali kununua ndege mbili mpya aina ya Bombardier Q 400 zitakazobeba
abiria 76 kila moja.
Magufuli alisema ndege hizo ni za kisasa na zinafaa kwa
safari za ndani, kwani zina uwezo wa kutua katika kiwanja chochote nchini
tofauti na Jet ambazo zinaweza kutua katika vi-wanja vitatu pekee.
Alisema ndege hizo zinatumia dakika 135 kutoka Dar es
Salaam hadi Mwanza huku Jet ikitumia dakika 145 na kuwa wanaoziponda hawana
hoja.
“Nasikia kuna watu wanaziponda ndege ambazo tunanunua,
lakini nataka kuwaambia kuwa ni nzuri ambazo tunaamini zitatumika katika
viwanja vyetu na kama mtu hataki kuzipanda apande za Jeshi zinazopita huko
nje,” alisema huku akimaanisha ndegevita ambazo jana zilikuwa zikiruka katika
anga la Dar es Salaam kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 52 ya Jeshi la Ulinzi
na Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Alisema tatizo la Watanzania ni kulalamikia jambo ambalo
linachangiwa na tabia iliyokuwepo huko nyuma ya kupiga dili ambazo nimeziziba.
Magufuli alisema kwa sasa dili hakuna, hivyo ni lazima
watu waanze kulalamika na kuwa hawezi kubadilika kusimamia Serikali, hivyo kila
mtu atakula kulingana na kazi ambayo anaifanya.
Alisema moja ya njia ambayo ametumia kuondoa dili katika
ofisi za Serikali, ni kubaini wafanyakazi hewa ambapo hadi jana walishabaini
wafanyakazi 16,500 ambao walikuwa wakipata fedha kinyume na taratibu.
“Kuna watu walikuwa wakikaa na kupanga mipango yao ya
kupiga dili, lakini kwa sasa haipo tena na ninawahakikishia kuwa wataaibika
sana, kwani mianya haipo,” alisema.
Alisema kutokana na hali aliyoikuta katika ‘upigaji
dili’, alitamani kubadilisha fedha ili watu waliohifadhi fedha za madili
wabakinazo huko huko.
“Yaani nchi hii ilikuwa ya dili, kila kona dili, hali ambayo
ilinisababisha kufikiria kubadilisha fedha ili wapiga dili wabakie na fedha zao
huko, lakini baadaye niliona niache tu,” alisema.
Halikadhalika, Rais Magufuli alitaka wahandisi nchini
wajipange kuhakikisha wanashiriki ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Tanga hadi
Uganda, kwani ni moja ya majukumu yao.
Uchumi wa viwanda
Akizungumzia wajibu wa wahandishi kuipeleka Tanzania
katika uchumi wa kati na viwanda, alisema jukumu hilo ni lao na kuwa hiyo ndiyo
sababu kubwa kuwateua katika nafasi mbalimbali.
Rais Magufuli alisema kwa muda mrefu amekuwa na imani na
kada hiyo, hivyo anaamini hawawezi kumwangusha katika jitihada zake ya kuifanya
Tanzania ya viwanda na uchumi wa kati.
“Nadhani mnaona Katibu Mkuu Kiongozi wangu ni mhandisi,
Mhandisi John Kijazi, Katibu wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa (Tamisemi) Mhandisi Mussa Iyombe na makatibu wakuu na naibu makatibu
wakuu,” alisema.
Rais alisema pia amefanya hivyo katika nafasi ya
mawaziri, naibu mawaziri, wakuu wa mikoa, makatibu tawala wa mikoa na nafasi
nyingine nyingi.
“Naamini mimi nimetimiza wajibu wangu kwa kuwapa nafasi
hivyo naomba mfanye kazi ili kuipeleka Tanzania katika uchumi wa kati na
viwanda mimi nitapambana na changamoto zingine kama ‘kutumbua majipu’ ya
wafanyakazi hewa,” alisema.
0 comments:
Post a Comment