Serikali yaeleza sababu za Mv D’SM kuegeshwa kambini


Suleiman Msuya

NAIBU Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani, amesema Kivuko cha Mv. Dar es Salaam, kitaanza kutumika baada ya mkandarasi kukamilisha marekebisho ambayo yanahitajika hasa kuhusu mwendo wa baharini.

Ngonyani aliyasema hayo jana wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii aliyetaka kujua sababu za kivuko hicho kilichoigharimu Serikali zaidi ya sh. bilioni 8 kuegeshwa katika kambi ya Jeshi la Majini Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Kivuko hicho cha MV. Dar es Salaam Kampuni ya Denmark iitwayo JGH Group (JGH Marine A/S/Johs. Gram-Hanssen A/S) ambapo baada ya kukamilisha matengenezo ilikabidhi Wakala wa Umeme, Mitambo na Ufundi (Temesa), lakini imegoma kukipokea kutokana na kuwa na mwendo mdogo.

Alisema kwa sasa kinachoendelea ni marekebisho hayo ambayo yakikamilika, kivuko hicho kitaanza safari.

Naibu Waziri Nngonyani alisema awali kivuko hicho kilikuwa kinapaswa kufanya kazi kutoka Dar es Salaam kwenda Bagamoyo, ila baada ya kukamilika upanuzi wa barabara ya Bagamoyo wanaona hakitakuwa na tija.

“Kivuko kimesimama kwa sababu kuna mapungufu ambayo yapo kinyume na mkataba, hivyo yakikamilika kitaanza kazi ila hakitaenda Bagamoyo,” alisema.

Aidha, alisema wizara ipo katika mkakati wa kujenga vivuko mbalimbali ambavyo vitatoa huduma katika maeneo tofauti nchini kama Kilombero, Tanganyika, Nyasa na Victoria.

Naibu Waziri Ngonyani amesisitiza mamlaka mbalimbali ambazo zinahusika na ujenzi wa barabara kuepuka kujenga matuta katika barabara hizo, kwani ni kinyume na utaratibu.

Alisema ni jambo la aibu kuona barabara zinatengenezwa kwa lami halafu zinawekewa matuta hali ambayo inasababisha magari kupata matatizo na kutembea mwendo ambao si sahihi.

Alitoa wito kwa wahandisi na wakandarasi kuhakikisha kuwa wanaweka alama za barabarani pale ambapo kunahitajika kuweka na si matuta.

Aidha, alisema ni vema presha za kisiasa kuepukwa katika kujenga barabara kwani inaonekana kuwa sababu ya barabara nyingi kujengwa kwa kuwekewa matuta.

Halikadhalika Naibu Waziriv Ngonyani amewataka wanananchi wa Kigamboni kuendelea kuwa na subira kwani suala la bei ya kuvuka daraja la Kigamboni linafanyiwa kazi.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo