Sheria ya habari yaanza kung’ata


Fidelis Butahe, Dodoma

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ametangaza kuanza kutumika kwa Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016 sambamba na kanuni zake zinazobainisha kiwango cha elimu kinachotakiwa kwa waandishi wa habari ni kuanzia stashahada na kuendelea.

Amesema kanuni hizo zimetoa kipindi cha mpito cha miaka mitano ya utekelezaji wa mambo mbalimbali, ikiwemo kiwango hicho cha elimu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana katika ukumbi wa Ofisi za Bunge mjini Dodoma, Nape alisema Sheria hiyo imeanza kutumika tangu Desemba 31 mwaka jana baada ya Rais John Magufuli kuisaini huku kanuni zake zikichapishwa katika Gazeti la Serikali (GN) la Februari 3 mwaka huu,

“Kipindi cha mpito kimeanza Januari mwaka huu hadi Januari mwaka 2021 kwa waandishi wasiokuwa na sifa za elimu wakasome. Sheria hii pia inaleta mfumo madhubuti wa kulinda haki za wanahabari kukusanya, kuhariri na kusambaza habari zao kwa uhuru. Vyombo vya habari sasa vitatekeleza haki yao hii ya kikatiba bila vikwazo visivyokuwa na sababu,” alisema Nape.

Alisema umma na wana tasnia wanakumbushwa sheria hii kwa lengo la kuwa na wanataaluma wanaotekeleza vyema wajibu wao na kama ilivyo kwa taaluma nyingine, imeweka wajibu kwa wale watakaokiuka msingi na maadili ya taaluma.

Alisema katika utekelezaji utekelezaji wa Sheria hiyo kwa taasisi zilizopo, zitaongezewa majukumu au kazi zake kuhuishwa sambamba na kuanzishwa kwa vyombo vipya.

“Jukwaa la Wahariri (TEF) walitoa maoni mazuri sana kuhusu suala la elimu. Tumechambua maoni yao na mengine. Wapo waliotaka iwe cheti, wengine shashahada, baadhi shahada na wapo waliotaka iwe shahada ya uzamivu. Pia wapo waliotaka iwe mtu yeyote anayejua tu kusoma na kuandika,” alisema Nape.

“Serikali imesimama katikati ya maoni yao. Sifa ya chini kabisa kwa kuanzia itakuwa ni stashahada ya uandishi wa habari. Hata hivyo Serikali imetoa kipindi cha mpito cha miaka mitano kwa wanahabari waliopo sasa na wanaotaka kuingia katika taaluma hii, ili wawe na sifa stahiki.”

Kuhusu kiwango cha elimu kwa wahariri wa habari alisema, “Nalo lilikuwa na mjadala mpana sana, lakini niwapongeze sana TEF waliwasilisha mapendekezo mazuri na sisi tukaona tuliache kwa wamiliki wa vyombo husika. Wao ndio wataamua.”

Alisema kanuni za sheria hiyo zinaeleza utekelezaji wake ikiwa ni pamoja na jinsi ya kuanzisha gazeti na masuala mengine huku akisisitiza kuwa vitambulisho vya waandishi wa habari vinavyotolewa kila mwaka na Idara ya Habari Maelezo vitaendelea kutolewa bila kuzingatia kiwango cha elimu hadi hapo kipindi cha mpito kitakapomalizika.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo