Wasomi wajadili JPM kutohudhuria miaka 40 ya CCM


Sharifa Marira na Charles James

WASOMI wametoa maoni tofauti kuhusu CCM kuadhimisha miaka 40 ya kuzaliwa bila Mwenyekiti wake, Rais John Magufuli na wenyeviti wastaafu kuwapo, wakisema hatua hiyo si nzuri kwa ustawi wa chama hicho tawala hasa kwa sasa.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Salim Hamad alisema suala hilo limeacha maswali mengi kutokana na kwamba si kawaida viongozi wakubwa kutohudhuria sherehe muhimu kama hiyo, ambayo pia hutumika kama njia ya kujenga chama na mambo mbalimbali hutokea wakati huo.

Alisema tatizo lililopo ni kwamba Dk Magufuli ni mtendaji, si mwanasiasa  hivyo anajaribu kufanya utendaji zaidi ili wananchi waiamini CCM na badala yake ameachia wasaidizi wake wafanye kazi .

“Ikiwa viongozi hao wameshindwa kuhudhuria sherehe za chama kwa sababu ya kubana matumizi si njia sahihi, kwani sherehe hizo si anasa ni njia ya kujenga chama na mara nyingi masikio ya Watanzania huwa kwenye eneo ambalo sherehe hufanyika,’’ alisema Hamad.

Profesa Benson Bana, kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alisema hali hiyo ni moja ya maboresho ambayo Mwenyekiti amekuwa akiyapigia kelele, inaonesha kuwa CCM ya sasa si ya matamko na matamshi.

“Sera ya Magufuli  ni kubana matumizi,  anaonesha vitendo si maneno na hiyo ndiyo CCM tuliyokuwa tunaitaka sherehe zinaweza kuwepo kwa njia yoyote ile, hata kwa kwenda shamba au kuhamasisha jambo zuri kwa jamii na zikafanyika vizuri Zaidi,’’alisema Profesa Bana.

Richard Mbunda alisema hakukuwa na maandalizi maalumu ya kuitangaza siku hiyo, matangazo ya kawaida yaliyozoeleka ya kuitangaza siku hiyo ya CCM hayakuwepo na ndiyo maana yameadhimishwa kimyakimya na hii imetokana na hali ya kisiasa ilivyo nchini, imesababisha kukosa msisimko kwa baadhi ya viongozi ndani ya chama.

Mbunda alisema sera ya Mwenyekiti wa chama hicho kubana matumizi inaweza kuwa sababu nyingine ya kutoshuhudia viongozi wakuu kuhudhuria maadhimisho hayo, kwani gharama zingekuwa ni kubwa zaidi tofauti na kuwakilishwa na viongozi wa chini.

“Ni wazi zile shamrashamra zimepotea na kutohudhuriwa huku kwa viongozi wakubwa kunaweza kuleta tafsiri hasi kwa wapenzi na wanachama ambao wanaweza kuhisi pengine viongozi wanasusa chama chao,” alisema Mbunda.

Ghamaly John ambaye ni msomi wa Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere alisema kutohudhuriwa huko kwa Rais Magufuli kunaweza kuwa ni mwendelezo wa staili yake ya kutofanya kazi kwa mazoea, kama ambavyo alionesha kwenye sherehe za Mapinduzi mwaka huu.

“Unajua Rais Magufuli amekuwa akionesha kwamba yeye si mtu wa kufanya kazi kwa mazoea ya miaka iliyopita, hivyo tusishangae akaibukia mkoa mwingine na kuadhimisha kwa staili ya aina yake.

“Lakini pia inatilia mkazo sera yake ya kubana matumizi ambapo kama angehudhuria yeye na Shein (Dk Ali Mohamed - Rais wa Zanzibar) pamoja na ujumbe wao gharama ingekuwa kubwa zaidi ikiwamo ya matangazo,” alisema Ghamaly.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo