Wake za viongozi waendelea kufariji wasiojiweza


Mwandishi Wetu, Tabora

MKE wa Rais, Mama Janeth Magufuli na Mke wa Waziri Mkuu Mama Mary Majaliwa wametoa mwito kwa Watanzania kujenga utamaduni wa kutembelea vituo vya wazee na watu wenye mahitaji maalumu na kutoa misaada ili kujikimu.

Walisema hayo jana walipotembelea makazi ya wazee wasiojiweza na walemavu watokanao na ukoma ya Amani Ipuli mjini hapa.

Katika makazi hayo walikabidhi tani 7.5 za vyakula ukiwamo mchele, unga wa sembe na maharage; pamoja na mafuta maalumu ya kujipaka watoto wenye ulemavu wa ngozi wanaosoma shule mbalimbali mkoani hapa.

Mama Magufuli alipongeza watumishi wanaofanya kazi kwenye makazi ya wazee na watu wenye mahitaji maalumu kwa sababu kazi hiyo ni ngumu na yenye changamoto nyingi.

“Ibada si kwenda nyumba za ibada pekee bali hata kutembelea wazee, watu wenye mahitaji maalumu na wasiojiweza, utakuwa umetoa sadaka kubwa kwa Mwenyezi Mungu.  Nawaomba tujitahidi kuwatembelea,” alisema.

Mama Majaliwa aliomba wananchi wawe na utaratibu wa kusaidia wazee wanaoishi kwenye makazi hayo, walemavu na wasiojiweza nchini na kuwafariji kwa sababu wanahitaji upendo na faraja zao.

Mwenyekiti wa Wazee waishio katika makazi hayo, George Busambilo aliwashukuru wake hao wa viongozi kwa niaba ya wenzake na kuwaomba waendelee na moyo huo wa kusaidia watu wasiojiweza na wenye mahitaji maalumu.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo