Viongozi wa dini waomba Makonda aongezewe ulinzi


Stella Kessy

BARAZA la Viongozi wa Dini la Kupambana na Dawa za Kulevya Tanzania lililo chini ya Tume ya Kupambana na Dawa za Kulevya, limeomba mamlaka husika kumuongezea ulinzi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kwa kuthubutu kutaja watuhumiwa wa dawa za kulevya.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Shekhe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Salum ambaye ni Mwenyekiti wa kamati hiyo, alisema ujasiri alioonesha Makonda kwa kujitoa mhanga kwa ajili ya Taifa na watu, umeonesha uthubutu unaohitaji kuungwa mkono.

"Sisi Baraza tunapinga vita na kulaani hatua yoyote ya kushiriki katika biashara au utumiaji wa dawa za kulevya, kwa kuwa matumizi ya dawa hizo yamekuwa kikwazo kikubwa cha maendeleo katika nchi yetu na yanapoteza nguvu kazi ya Taifa huku waathirika wakubwa wa matumizi ya dawa hizo wakiwa vijana,"alisema.

Alifafanua kuwa endapo kiongozi wa dini atabainika kushiriki katika matumizi ya dawa za kulevya, Baraza litamwita na kumuonya ili ajiepushe na dawa zilizoangamiza vijana wengi hapa nchini.

Shekhe Salum alisema kutokana na ugumu wa kazi hiyo, wanaendelea kumwombea Mungu ili Makonda afanyekazi hiyo kwa ukamilifu itakayosaidia kukomboa nguvu kazi ya Taifa ambayo waliowengi ni waathirika wa matatizo ya dawa za kulevya.

"Kutokana na ugumu wa kazi hiyo tunamwombea kwa Mwenyezi Mungu ili ampe ulinzi na kinga, pia azidi kumpa moyo wa uajsiri wa kupambana na maovu yote yanayoharibu sifa ya Taifa letu na vijana wetu," alisema.

Aliwaomba wananchi wote kumuunga mkono na kumpa ushirikiano wa kutosha Makonda kwa uthubutu ambao ameonesha ili kujenga Taifa imara la wachapakazi.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo