Vijiji vyote kupatiwa umeme ifikapo 2030


Salha Mohamed

ASILIMIA 100 ya vijiji vinatarajiwa kunufaika na nishati ya umeme ifikapo 2030.

Mkurugenzi Mkuu Wakala wa Nishati Vijijini (Rea), Boniface Gissima, alisema hayo jana katika taarifa yake kuhusu utekelezaji wa shughuli za Wakala huyo za usambazaji wa umeme katika vijiji 7,873 Tanzania Bara.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Awamu ya Tatu ya mradi wa kusambaza umeme itatekelezwa katika vijiji hivyo kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka huu wa fedha   hadi 2020/2021.

“Kati ya vijiji hivyo, vijiji 7,697 vitapelekewa umeme wa gridi na vijiji 176 umeme wa nje ya gridi na utekelezaji wake utajumuisha kuongeza wigo wa miundombinu ya usambazaji umeme,” alisema.

Alisema katika utekelezaji wa kuongeza wigo wa miundombinu ya usambazaji umeme, tayari umeanza baada ya kusainiwa kwa mkataba wa miradi hiyo Desemba mwaka jana katika mikoa sita itakayogharimu dola za Marekani milioni 27.

Alisema mradi wa usambazaji wa vijiji 305, utagharamiwa kwa fedha kutoka serikali ya Tanzania na Norway.

Gissima alisema ili kufikisha umeme katika vijiji 3,559 ambavyo havijafikiwa na miundombinu ya umeme wa gridi, Serikali inatarajiwa kutumia Sh. Bilioni 733.98.

“Katika miundombinu hii, mradi utatekelezwa katika muda wa miezi 24 kuanzia mwaka wa fedha 2016/2017 hadi 2017/2018. Taratibu za ununuzi zinaendelea na wakandarasi wataanza kazi Aprili mwaka huu,”alisema.

Alisema hadi sasa vijiji 4,395 kati ya vijiji 12,268 sawa na asilimia 36, wameunganishwa na huduma ya umeme na hadi kukamilika kwa mradi huo, vijiji 7,934 sawa na asilimia 65 vitakuwa vimefikiwa na mradi huo.

Gissima alisema vijiji vitakavyosalia, vitapelekewa umeme mwaka wa fedha 2018/2019 hadi 2020/2021 kadri upatikanaji wa fedha utakavyoruhusu.

Katika hatu nyingine, Gissima alisema dola za Marekani milioni 84, zimetengwa kwa ajili ya mradi wa kusambaza nishati jadidifu kwenye maeneo yaliyombali na gridi na visiwa vilivyo kwenye maziwa na Bahari ya Hindi.

“Katika mradi huu, dola milioni 42 zimetolewa na Benki ya Dunia, ambapo wakala ilitangaza Awamu ya Kwanza ya mradi Septemba 23, mwaka jana na awamu ya pili itatangazwa April mwaka huu,” alisema.

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo