Wenyeviti Dar waanika vijiwe vya mihadarati


*Viko maeneo wanakoishi vigogo kisiasa, kiuchumi

*Walalamikia polisi kushiriki na ‘wazungu wa unga’

Enlesy Mbegalo

Baadhi ya watuhumiwa mihadarati
IKIWA ni siku ya pili tangu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuwapa siku 10 wenyeviti wa serikali za mitaa   kutoa taarifa za nyendo za wanaojihusisha na dawa za kulevya, wenyeviti hao wametaja vijiwe mama vya uuzaji na utumiaji mitaani kwao.

Wenyeviti hao wa mitaa ya Oysterbay, Kunduchi, Kawe na Magomeni, wamesema vita hivyo vinawezekana na wanachohitaji ni ushirikiano zaidi kutoka Serikali Kuu, Polisi na Mkoa.

Baadhi ya wenyeviti hao walisema vita hivyo vilikuwa vigumu kutokana na baadhi ya polisi wasio waaminifu kuchukua rushwa, kujihusisha na uuzaji, kutumia dawa hizo na ‘kutembea’ na wasichana wanaojiuza kwa kuwa baadhi yao hutumia na kuuza mihadarati hiyo.

Ukwamani
Mwenyekiti wa Ukwamani, Sultani Jetta alisema mtaa wake umekuwa ukitumika kwa uuzaji wa mihadarati na amekuwa akikemea mara kwa mara na kutoa taarifa Polisi Kawe lakini wahusika wamekuwa wakikamatwa na kutolewa.

“Tamko la Mkuu wa Mkoa Makonda limekuja kwa wakati mwafaka kwangu, kwani nimepambana sana na vita hivi, baada ya kuona vijana wengi mtaani kwangu wanaangamia, ila sikuwahi kupata msaada zaidi ya hawa watu kuwekwa ndani na baada ya siku tatu kutolewa,” alisema Jetta.

Alisema eneo maarufu ambalo limekuwa likitumika ni la soko la zamani, ambalo ni maarufu sana kwa uuzaji na utumiaji wa mihadarati hiyo.

“Kwa kuwa biashara ya dawa za kulevya inahusisha baadhi ya askari na tayari kwenye kituo chetu cha Kawe kuna mmoja wao amesimamishwa kazi kwa tuhuma hizo, hivyo imani yangu ni kwamba yawezekana kuna wengine watajitokeza kupambana kinafiki ili kujisafisha wakati ni miongoni mwao,” alisema Jetta.

Aliongeza: “Binafsi orodha nilishaikabidhi muda mrefu kituo cha Kawe na hakuna jipya na orodha hiyo ya majina nitaipeleka   kwa Mkuu wa Mkoa kwa kuwa ameonesha nia ya dhati ya kupambana.”

Alisema alipata kutoa taarifa kwenye kituo hicho kuhusu polisi maarufu anayetuhumiwa kama kibaraka wa wauza ‘unga’ mara kwa mara kwenye kijiwe cha mtaa wake, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa.

“Nadiriki kusema baadhi ya askari wa muda mrefu katika kituo cha Kawe ni vichaka vya wauza dawa za kulevya na nimekuwa nikipokea malalamiko mengi kutoka kwa wazazi wa maeneo ya kijiwe hicho, kwa jinsi wanavyopishana kupokea hongo,” alisema na kuongeza:

“Hivyo nawaomba wenyeviti wenzangu wa mkoa huu, tuwe wakweli bila kuficha maana hili ni janga kwa vijana wetu.”

Kunduchi
Mwenyekiti wa mtaa wa Kunduchi, Richard Rusisye alisema katika mtaa wake, kuna vijiwe vya uuzaji na utumiaji dawa za kulevya yakiwamo maeneo ya Meko Uwanja wa mpira, Kokoni na Pwani.

“Eneo la Kokoni ni ambalo linatumika na watu wengi kutoka sehemu mbalimbali za Jiji na polisi wakienda kuwakamata hukimbilia kwenye mikoko, kwani eneo hilo ni la mikoko,” alisema.

Rusisye alisema pia kuna baadhi ya baa kwenye mtaa wake ambazo zimekuwa zikitumika kuuza na matumizi ya mihadarati hiyo.

Oysterbay
Mwenyekiti wa mtaa wa Oysterbay, Zefrin Lubuva alisema ukanda wa Barabara ya Haile Salassie ni kero kutokana na watumiaji na wauzaji wa dawa za kulevya, pia baa bubu alizosema zinachangia kukithiri kwa biashara hiyo.

Lubuva alisema kabla ya tangazo la Serikali, waliendesha operesheni mtaani kwake na kubaini watu kujificha kwenye biashara ndogondogo ukiwamo  uuzaji wa pombe za ‘viroba’.

“Tuko pamoja na Mkuu wa Mkoa kwenye vita hivi vikubwa ambapo nguvukazi ya Taifa hili, vijana, wanaangamia huko na tutatoa taarifa, kwani unakuta kuna watu wanafanya kazi za kung’arisha viatu, kumbe wanajihusisha na biashara hizo,” alisema

Aliongeza: “Nimepiga marufuku biashara ya ‘viroba’ kwenye mtaa wangu na uwepo wa bajaji.”

Mzimuni
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mzimuni, Hassan Ngonyani alitaja maeneo yanayotumika kuuza na kutumia dawa za kulevya kuwa ni Tanganyika Packers, Maringo, Mikoroshini, bustani za maua na karibu na ukuta wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kambi ya Lugalo.

Pia baadhi ya wenyeviti walisema vita hivyo vinahitaji uthubutu wa hali ya juu, kwani ni vikubwa na vinajulikana na baadhi ya polisi ambao wamekuwa wakichukua rushwa kwenye vijiwe hivyo.

“Maeneo mengi polisi wamekuwa wanafeli kutokana na kupokea rushwa, kuuza, kutumia na kujenga urafiki na wauza mihadarati,” alisema mmoja wa wenyeviti ambaye hakuwa tayarin kutaja jina lake.

Hata hivyo, baadhi yao walisema wameanza kupokea simu kutoka kwa wahusika wakiwasihi wasiwataje itakapohitajika orodha ya majina ya watumiaji na wauzaji mihadarati hiyo.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo