Zitto aokolewa na Ndugai usiku

Fidelis Butahe, Dodoma

Zitto Kabwe
KITENDO cha Jeshi la Polisi kutaka kumkamata Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe, juzi baada ya kutoka bungeni, kilimfanya mbunge huyo kuondoka bungeni usiku wa manane kuamkia jana kwa msaada wa Spika wa Bunge, Job Ndugai.

Juzi, wakati Zitto akiwasilisha hoja bungeni kuhusu utaratibu wa wabunge, hasa wa upinzani kukamatwa na polisi bila utaratibu, alibainisha kuwa hata yeye amepewa taarifa kuwa akitoka nje ya viwanja vya Bunge atakamatwa, kuahidi kulala bungeni ili kuwakwepa polisi.

Baada ya wabunge wa upinzani kususia kikao cha Bunge juzi saa 10:30 jioni kutokana na hoja hiyo kupingwa na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson,  Zitto aliendelea kuwepo ndan  ya eneo la Bunge hadi jana saa 6:25 usiku alipoondoka kwa msaada wa Ndugai aliyempatia usafiri.

Hata hivyo, kususia kikao kwa wabunge hao wa upinzani sambamba na Zitto kusakwa na polisi, jana asubuhi kulimfanya Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge kutaka Serikali na Bunge kufanya kazi kwa pamoja, huku akisema taarifa ya kukamatwa hovyo kwa wabunge ataifikisha kwa Ndugai  aliyedai kuwa ataitolea tamko rasmi leo.

Zitto asimulia

“Niliondoka saa 6 usiku ikiwa ni baada ya mashauriano kati yangu na Katibu wa Bunge (Dk Thomas Kashilillah) na Spika Ndugai  ambaye aliwasiliana na IGP (Mkuu wa Jeshi la Polisi-Ernest Mangu),” alisema Zitto.

“Nilivyokuwa nawasilisha hoja yangu bungeni nilikuwa najua kila kitu juu ya kukamatwa kwangu ndio maana nikaamua kutotoka bungeni kwani walikuwa wakinisubiri nje ya viwanja wa bunge.”

Alisema baada ya majadiliano ya muda mrefu, IGP aliwasiliana na Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, Lazaro Mambosasa ambaye alibainisha kuwa mbunge huyo alikuwa akitafutwa kwa kutoa kauli uchochezi alipokuwa mkoani Shinyanga, kubainisha kuwa polisi ilikiri kutoona kosa lake.

Alisema baada ya mashauriano hayo alihakikishiwa kuwa akitoa hatokamatwa na polisi lakini kwa kujihami zaidi Spika Ndugai alituma usafiri wa kumchukua.

“Spika aliwasiliana na mkuu wa ulinzi wa Bunge ili kuniwezesha kutoka salama ila pamoja na kuwasiliana naye bado alinitumia gari ambalo lilinitoa ndani ya viwanja vya Bunge,” alisema.

Juzi mpaka saa tatu baadhi ya mageti ya kutoka na kuingilia ndani ya Bunge kulikuwa na magari ya polisi huku ulinzi ukiwa umeimarishwa kwa kiwango kikubwa.

Kauli ya Mwenyekiti wa Bunge

Jana wakati akijibu mwongozo wa mbunge wa Tarime Vijijini(Chadema), John Heche kuhusu polisi kuwakamata wabunge bila utaratibu, Chenge alisema polisi wanaweza wasiwakamate wabunge pindi vikao vya Bunge vinapokuwa vikiendelea, badala yake kufanya hivyo wakati mwingine.

Katika maelezo yake, Chenge alisema kuna haja pia ya kuimarisha uhusiano kati ya Serikali na Bunge kwa kuwa mihimili hiyo ina majukumu yanayofanana.
“Heche nimekusikia ingawa hukueleza kwa undani, lakini najua suala hili lilianza jana na Naibu Spika akalitolea ufafanuzi,” alisema.

“Ushauri wangu katika hili, kuna haja ya kuwa na mahusiano mazuri kati ya Bunge na Serikali, lakini pia nakuomba Heche umwandikie Katibu wa Bunge umweleze mapendekezo yako ili yafikishwe katika Kamati ya Bunge ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge kwa mjadala zaidi.

Alisema baada yah apo uongozi wa Bunge unaweza kujadiliana na Serikali kwa sababu kama polisi wanamhitaji mbunge, wanaweza kusema wa wakamkamata wakati mwingine kwa sababu wanajua anapoishi.

Awali, Heche alisema kama Bunge halitachukua hatua pindi wabunge wanapodharirishwa, utafika wakati Bunge litaanza kudharirishwa.

Alisema Bunge ni chombo kinachoheshimika duniani kwa sababu kinatunga sheria na kupitisha bajeti ya Serikali lakini hivi sasa heshima yake.

 “Hii tabia ya wabunge kukamatwa ovyo, tena bila taarifa ya Spika, haipendezi na hata wakuu wa wilaya wanawanyanyasa sana wabunge huko majimboni. Kwa hiyo, naomba mwongozo wako mheshimiwa mwenyekiti ili uniruhusu niwasilishe hoja yangu ili Bunge liijadili,” alisema Heche.

Wabunge walivyotoka bungeni

Juzi, wabunge wa upinzani, walitoka nje ya Bunge wakionyesha kutoridhishwa na majibu ya Naibu Spika, Dk. Tulia Akson, aliyoyatoa wakati alipokuwa akijibu taarifa ya kukamatwa kwa wabunge wa upinzani iliyowasilishwa na Zitto.

Katika taarifa hiyo, Zitto aliwataja wabunge wa Chadema, Godbless Lema wa Arusha Mjini aliyeko mahabusu katika Gereza la Kisongo, Arusha kwa zaidi ya miezi mitatu sasa, Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali anayetumikia kifungo cha miezi sita katika Gereza la Ukonga Dar es Salaam na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu anayeshikiliwa na Jeshi la Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam.

Hata hivyo, wakati Dk. Tulia akijibu taarifa hiyo, alisema kanuni za Bunge zinataka Spika wa Bunge apewe taarifa za kukamatwa mbunge aliyetenda makosa ya madai na kama siyo makosa ya madai, hakuna haja ya spika kupewa taarifa.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo