Profesa Mwandosya kuibuka upya


Mwandishi Wetu

Profesa Mark Mwandosya
BAADA ya ukimya wa muda mrefu, mwanasiasa mkongwe na Waziri wa Maji mstaafu, Profesa Mark Mwandosya, anatarajiwa kuibuka katika maadhimisho ya Siku ya Nile, jumatano wiki hii.

Profesa Mwandosya ametajwa kuwa mmoja wa wazungumzaji wakuu katika maadhimisho hayo ya yatakayofanyika jijini Dar es Salaam yakihusisha mawaziri wa maji wa nchi 10 wanachama wa Bonde la Mto Nile, ambapo Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan atakuwa mgeni rasmi.

Ushiriki wa Profesa Mwandosya katika mkutano huo unatajwa kuwa tukio la kwanza la hadhara tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa 2015 alipojaribu kuwania urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), lakini kura za maoni hazikutosha.

Hivyo Profesa Mwandosya anatarajiwa kuvuta hisia za wengi, hasa baada ya kukosekana kwenye majukwaa ya kisiasa na kijamii tangu mwaka juzi.
Katika maadhimisho hayo, mambo mbalimbali yanatarajiwa kujadiliwa ikiwamo umuhimu wa Mto Nile katika kuzipatia nchi wanachama maji, chakula na umeme wa uhakika.

Mahitaji hayo yatatolewa kupitia miradi endelevu tofauti inayofaidisha nchi wanachama kupitia rasilimali zake chini ya Taasisi Inayosimamia Shughuli za Nile (NBI).

Naibu Mkurugenzi wa Maji katika Wizara ya Maji na Umwagiliaji inayoandaa maadhimisho hayo, Sylvester Matemu alisema Profesa Mwandosya amepewa nafasi hiyo kutokana na uzoefu wake na utaalamu katika sekta ya maji.

Pia Matemu alisema Profesa Mwandosya amefanya utafiti na kuandika kitabu kuhusu Mto Nile.

“Pamoja na Mwandosya, mawaziri wote wa maji kutoka nchi wanachama watazungumza katika maadhimisho hayo ya kihistoria,” alisema Matemu katika mkutano wake na wahariri wa vyombo vya habari kuhusu maadhimisho hayo mwishoni mwa wiki.

Alisema maadhimisho hayo yatafanyika Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere ukishuhudia pia upandaji miti, ambao utatanguliwa na maandamano yatakayoanzia Viwanja vya Mnazi Mmoja.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa NBI, Mhandisi Innocent Ntabana alisema madhimisho ya siku hiyo alitaja nchi wanachama kuwa ni Tanzania, Kenya, Uganda, Sudan, Sudan Kusini na Kongo.

Nyingine ni Ethiopia, Burundi, Rwanda na Misri ambapo Ntabana alieleza kwamba maadhimisho hayo yatatumika pia kama jukwaa la majadiliano kwa nchi hizo kuhusu rasilimali maji ya Mto Nile, mikakati ya kuifanya endelevu na kukabili changamoto za kimazingira zilizopo ili liendelee kuhudumia mamilioni ya watu wanaotegemea mto huo.

Profesa Mwandosya amekuwa kimya kwa zaidi ya mwaka mmoja tangu kumalizika kwa mchakato wa kutafuta mgombea urais ndani ya CCM mwaka 2015, ambapo wagombea zaidi ya 35 akiwamo yeye walijitokeza na kuchujwa hatua za awali.

Hali hiyo iliyozua malalamiko kutoka baadhi ya wajumbe hata baadhi kuamua kujitoa CCM akiwamo Waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa aliyehamia Chadema.

Katika mchakato huo, Rais John Magufuli alipitishwa kabla ya kuchaguliwa katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 30 mwaka jana akimshinda mpizani wake wa karibu, Lowassa.

Lowassa aliwania nafasi hiyo kupitita Chadema na kuungwa mkono na vyama vinne vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi(Ukawa).

Mara kadhaa gazeti hili limekuwa likimtafuta Mwandosya aliyewahi kuwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji katika Serikali ya Awamu ya Nne na pia Waziri Asiye na Wizara Maalum ili kupata maoni yake kuhusu masuala mbalimbali lakini mara azote simu yake imekuwa ikiita bila kupokelewa.

Ukimya wa Profesa Mwandosya ulizua maswali mengi, lakini Desemba mwaka jana alipopigiwa simu na gazeti hili ili kuzungumzia pamoja na mambo mengine mwaka mmoja wa Serikali ya Rais ya Awamu ya Tano na CCM, alisema hana cha kusema.

“Mimi nipo kijijini kama unataka kujua masuala ya kijijini kwangu niulize hayo ya mwaka mmoja wa Magufuli na CCM sina ‘coment’ kwa sasa nafanya shughuli zangu kijijini na kupumzika,” alisema.

Mwandosya anatajwa kama moja ya viongozi waliofanya kazi kwa mafanikio huku akionesha utulivu na kujiamini kwa kila jambo hasa bungeni ambapo alikuwa akitumia msemo wa kisomi kwa kuwataka wabunge watoe hoja na si kufoka katika jambo wasilolijua.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo