Wananchi kumfuata Waziri Mkuu Dodoma


Peter Kimath, Mvomero

Kassim Majaliwa
WANANCHI wa Kitongoji cha Majichumvi Kijiji cha Wami-Luhindo wilayani hapa mkoani Morogoro, wanakusudia kumfuata Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ofisini kwake mjini Dodoma ili kumweleza namna viongozi wilaya na mkoa walivyoshindwa kutekeleza agizo lake la kutatua migogoro ya ardhi.

Walisema viongozi hao wameshindwa pia kuainisha mashamba pori na kuwasilisha taarifa kwa Waziri Mkuu.

Mkuu wa mkoa, Dk. Steven Kebwe alikiri kuwepo agizo hilo akifafanua kuwa lilielekezwa zaidi kwa Mkurugenzi wa halmashauri kwani ndiye msimamizi wa maendeleo na ana fungu la fedha za kukabiliana na changamoto za maendeleo kwa jamii.

“Nikuombe usubiri nimtafute ili atupe majibu ya tatizo hili. Ni kweli nakumbuka siku hiyo baada ya uzinduzi wa kiwanda tulikutana na wananchi na Waziri Mkuu alizungumza nao na kutoa maelekezo kama hayo kwa mkurugenzi wa halmashauri,”alisema Dk Kebwe.

Majaliwa alitoa agizo hilo Agosti 3, mwaka jana baada ya kusimamishwa njiani na wananchi wa eneo hilo wakati akitoka kuzindua Kiwanda cha Nyama Mguluwandege Manispaa ya Morogoro.

Mbele ya mkutano maalumu wa kitongoji uliohudhuriwa na Katibu wa CCM Wilaya ya Mvomero, Amosi Shimba, Mwenyekiti wa kijiji, Apolinari Kahumba na Mwenyekiti wa kitongoji, Michael Mayala ambapo ilielezwa kuwa agizo la Waziri Mkuu limepuuzwa na kusababisha zaidi ya watoto 150 kukosa elimu na wengine 50 kuishia kufanya kazi za ndani, kuoa na kuolewa.

“Kama ilivyo kwenye historia yetu eneo hili tuliletwa na Serikali baada ya kuhamishwa kilipo Kiwanda cha Nyama Mguluwandege, tukaliendeleza kwa kuweka alama na kuweka huduma za kijamii, kuanza ujezi wa shule ya msingi iliyozinduliwa na aliyekuwa Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla mwaka 2014 pia majengo ya ibada” alisema Mayala.

Mwenyekiti huyo alifafanua kuwa wakati wakiendelea kujiimarisha walianza kupokea taarifa zilizoongezewa nguvu na mkurugenzi wa wilaya hiyo kuwa ingawa eneo hilo halijaendelezwa linamilikiwa na mtu ambaye hakutajwa akiwa na hati hivyo wao wajiandae kuondoka muda wowote.

Mbali na kutaka kumfuata Majaliwa Dodoma, wananchi hao wameeleza kusikitishwa na Serikali kwa kushindwa kukamilisha vyumba viwili vya madarasa na ofisi ya walimu viliyojengwa miaka minne iliyopita hadi pamoja na kero mbalimbali ikiwamo ukosefu wa huduma za kijamii yakiwemo maji, shule, soko, makaburi na majengo ya ibada.

Katika hatua nyingine, Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) kupitia Mchungaji wake James Mabula limetoa idhini kwa wananchi kutumia jengo la kanisa lake kama chumba cha darasa katika kipindi hiki ambapo jamii inasubiri suluhu dhidi ya mtu anayetajwa kuwa eneo ni lake.



Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo