Watumishi 2 TRA mbaroni kwa ‘mihadarati’


Salha Mohamed

WATUMISHI wawili wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wamekamatwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, kwa madai ya kupitisha kemikali bashirifu.

Kemikali hizo ni aina ya ephedrine, ambazo hutumika kutengezea dawa za kulevya aina ya heroin.

Kamishna wa Operesheni wa Mamlaka hiyo, Mihayo Msikhela alisema jana Dar es Salaam, kuwa watuhumiwa hao walikamatwa kwenye operesheni ya siku nne na wengine wawili wanasakwa na Mamlaka hiyo.

“Watumishi hawa wawili tayari tunao na taratibu zinafuatwa na muda wowote watafikiswa mahakamani, bado wawili tunaendelea kufuatilia nyendo zao,” alisema.

Alisema msako unaendelea nchi nzima dhidi ya wakulima, waingizaji, wasambazaji na watumiaji wa dawa za kulevya, za mashambani na  viwandani.

Kamishna Msikhela alisema dawa za kulevya za mashambani ni kero kubwa nchini na kwamba walipokabidhiwa hati ya watu wanaojihusisha na biashara hiyo, baadhi ya watuhumiwa walibainika kuwa watumishi wa umma.

Msikhela alisema mikoa ya Tanzania Bara imeonesha mafanikio makubwa katika kubaini na kuteketeza mashamba ya dawa za kulevya aina ya bangi na mirungi.

Alitaja mkoa wa Tanga kuteketeza mirungi kilo 44 na bangi puli tatu, Morogoro bangi kilo 18 na heroin kete tatu, Shinyanga bangi kilo 10, Kagera ekari 14 za bangi na mirungi ekari moja.

Mikoa mingine ni Njombe bangi nusu ekari, Songwe heroin kete 274 mirungi kilo tatu, Tabora bangi kilo sita, Singida bangi misokoto 203 heroin kete moja.

Aliongeza kuwa mkoa wa Rukwa bangi kete 105, Mbeya bangi kilo tano, Kigoma bangi nusu ekari, Lindi bangi gramu 496 na heroin kete 50.

Mkoa wa Simiyu uliteketeza bangi ekari 40, Ruvuma bangi gramu 300 na Tarime Rorya bangi ekari 36.

“Kati ya hii, mkoa uliofanya vizuri zaidi katika ukamataji dawa za kulevya za mashambani ni Simiyu kwa kuteketeza mashamba ya ekari 40,” alisema.

Alisema kwa dawa za viwandani, mkoa uliofanikiwa kukamata dawa za kulevya nyingi ni Lindi iliyokamata kete 50 na unafanyika utaratibu wa kuzipeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, huku watuhumiwa wakiendelea kuhojiwa.

Alisema hadi sasa watuhumiwa waliokamatwa kwa dawa za kulevya ni wengi huku akibainisha kuwa watalitolea ufafanuzi.

Alipongeza wananchi waliotoa taarifa za wauzaji na watumiaji dawa hizo akisema kunaonesha mafanikio huku akiwa na imani ya Tanzania bila dawa za kulevya kuwezekana.

Aidha, Msikhela alipotakiwa kutaja majina ya watumishi waliokamatwa alisema kutaja majina si sahihi.

Alipotakiwa kutaja orodha aliyokabidhiwa kama kuna watoto wa vigogo au la, alisema: ” Naomba kukuhakikishieni kwamba yeyote aliyetajwa kwenye orodha ataguswa hatutazami kigogo ni yupi na yupi si kigogo yaliyomo mle ni majina ya wahalifu kama wahalifu wengine”.

Mbali na hilo, Mihayo alisema katika orodha ya majina 97 waliyokabidhiwa hivi karibuni na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kama kuna waliokamatwa, alisema bado wanafuatilia na watatoa taarifa.

Alipotakiwa kutofautisha kiutendaji kati ya utajaji majina kwa awamu ya kwanza na ya pili, na hata ya tatu, alisema kutaja na kutotaja yote ni mifumo ya uhakikishaji, kwamba makosa yanayosumbua mitaani hayaendelei kusumbua tena.

Alisema yapo makosa ya wazi na yaliyojificha, hivyo ya wazi itajulikana yako kwenye hatua ipi na yaliyojificha hatua ipi na yanafuatiliwa kwa mfumo upi.

Aliulizwa endapo ikithibitika Makonda hakufuata utaratibu wa kutaja majina kama atachukuliwa hatua, alishindwa kujibu swali hilo huku akiwataka waulizaji kuangalia mifumo ya maswali ilivyo.

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo