Nape amkosoa Makonda


Fidelis Butahe, Dodoma

Nape Nnauye
SIKU nne baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kuwataja wasanii kadhaa wa muziki wa kizazi kipya na filamu akiwatuhumu kuhusika kwa namna tofauti na biashara ya dawa za kulevya, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, amesema ni makosa kuwahukumu moja kwa moja kuwa wanajihusisha na biashara hiyo.

Nape amesema licha ya kuunga mkono juhudi za kupambana na biashara na matumizi ya dawa za kulevya, busara inapaswa kutumika katika kuwabainisha watuhumiwa kwa sababu bado hawajahukumiwa na Mahakama.

“Ni muhimu kulinda haki ya mtuhumiwa, jambo lenye mjadala ni busara inayotumika kushughulika na wahusika ili kusaidia vyombo vingine kuwataja wanaosambaza,” alisema Nape jana katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini hapa.

“Tusiwahukumu kwa tuhuma maana wasanii kujenga brand (kujenga jina) ni kazi kubwa ila kubomoa jina ni sekunde tu. Ni sawa na kusema huyu kichaa, lazima jamii itamchukulia ndivyo sivyo.”

Februari 2 mwaka huu, Makonda aliwataja wasanii kadhaa pamoja na askari polisi 12 kwa tuhuma za kuhusika na biashara ya dawa za kulevya. Mpaka sasa takribani wasanii saba wameshahojiwa, huku askari hao wakisimamishwa kazi kupisha uchunguzi dhidi yao.

Wasanii wanaochunguzwa kwa tuhuma hizo ni Khalid Mohamed (TID), Dogo Hamidu, msanii wa filamu nchini, Wema Sepetu na Babuu wa Kitaa ambaye pia ni mtangazaji wa Televisheni ya Clouds.

Wengine ambao wametakiwa kufika kituo Kikuu cha Polisi kwa ajili ya kuhojiwa ni mwanamuziki, Vanessa Mdee na Tunda Sabasita.

Tangu kuibuka kwa sakata hilo, wadau mbalimbali wamekuwa wakikosoa utaratibu uliotumika kwa maelezo kuwa wasanii hao wanahukumiwa kabla ya uchunguzi kufanyika ili ibainike kama wanajihusisha na biashara hiyo ama la.

“Ni vizuri tukaangalia, tufanye katika namna ya kumlinda mtuhumiwa ili hata kama hausiki jina lake lisiporomoke,” alisema Nape.

“Matumizi ya dawa za kulevya yanaathiri wadau wetu ndio maana tumekuwa tukifanya juhudi za kuwasaidia kuwapeleka katika vituo maalumu vya kuwasaidia kuondokana na matumizi ya dawa hizi.”

Mbunge huyo wa Mtama alisema licha ya juhudi za kupambana na dawa za kulevya, kumekuwa na sintofahamu kuhusu sheria ya dawa za kulevya kutosema chochote kwa anayetumia.

Alisema wapo watu wa kada mbalimbali wanaotumia dawa za kulevya, lakini wasanii wanaonekana zaidi kwa kuwa ni maarufu na kubainisha jinsi Serikali kupitia wizara yake inavyowasaidia kuondokana na matumizi ya dawa za kulevya, akiwemo msanii Rehema Chalamila maarufu kama Ray C.
“Matumizi ya dawa za kulevya ni tatizo la jamii nzima, mapambano lazima yaanzie kwenye familia zetu. Hawa watu wanahitaji msaada kama ilivyo kwa wagonjwa wengine,” alisema Nape.

Alipoulizwa nini suluhisho la utaratibu unaotumika kuwataja na kuwahusisha moja kwa moja wasanii na biashara hiyo alisema, “tuache jamii ijadili.”

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo