TCRA yazindua huduma ya kuhama mtandao


Abraham Ntambara

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imezindua elimu kwa umma kuhusu huduma ya kuhama kutoka mtandao mmoja wa simu kwenda mwingine bila kubadili namba ya simu ya kiganjani.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo jana Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu, James Kilaba alisema huduma hiyo itamuwezesha mteja kubaki na namba yake bila kujali mtandao anaotumia, kwani anapoamua kuhama huhama nayo kama ilivyo.

“Mteja hana haja ya kusumbuka kuwataarifu watu wake wa karibu, marafiki, familia na wafanyakazi wenzake au washirika katika shughuli zake kwamba amebadilisha namba kwani inabakia ile ile,” alisema Kilaba.

Aidha alisema huduma hiyo kwa Bara la Afrika imeanzishwa pia nchini Misri, Kenya, Sudani, Afrika Kusini, Ghana, Nigeria, Senegal na Morocco.

Aliongeza kuwa nchi za Rwanda, Namibia na nyinginezo zipo katika mchakato wa kuanzisha huduma hiyo pia.

Kilaba alifafanua kuwa uanzishwaji wa MNP ni kwa mujibu wa kanuni za mwaka 2011 (Electronic and Postal Communications) Regulations, 2011) za uanzishwaji wake ambapo alisema kuwa kanuni hizo zinawataka watoa huduma za simu za kiganjani kuwezesha huduma hii katika mitandao yao.

Alisema katika utekelezwaji wake, TCRA imewashirikisha watoa huduma za kibenki ili wafunge mifumo itakayotambua namba zilizohama na hivyo kuwa na uwezo wa kutuma fedha mitandaoni bila shida yoyote.

Kilaba alisema faida za huduma hii ni nyingi, ikiwamo kuongeza ushindani kwenye sekta ya mawasiliano na hivyo kuwa kichocheo cha utoaji huduma bora kwani bila huduma nzuri wateja watahama.

Aliongeza nyingine ni kumpa uhuru mtumiaji wa huduma za simu za viganjani kuchagua mtoa huduma ambaye anaona anatoa huduma bora Zaidi.

Alisema TCRA imeandaa program ya kuelimisha wananchi juu ya mfumo huu ambapo elimu hii itafanyika kupitia vipindi vya redio, televisheni na kwa njia ya vipeperushi mbalimbali.

Alisema kupitia vipindi hivyo wananchi wataelimishwa namna ya kuhama pamoja na vigezo na masharti yake. Pia wataelimishwa haki zao wakati wa kuhama.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo