India yaingilia kati raia waliokamatwa


*Balozi asema tatizo mawasiliano mabovu Uhamiaji
*Afuatilia ili kumaliza mtafaruku huo kidiplomasia

Leonce Zimbandu

SIKU chache baada ya Idara ya Uhamiaji kukamata raia wa India kwa madai ya kufanya kazi bila vibali, Balozi wa India nchini, Sandeep Arya, ameingilia kati suala hilo na kusema tatizo lilikuwa mawasiliano kati ya mwajiri na Uhamiaji.

Akizungumza jana na mwandishi wa gazeti hili, Balozi Arya alisema anaendelea kufuatilia kwa karibu suala hilo na kudokeza kuwa jitihada  za kumaliza sintofahamu hiyo, zinaendelea kwa njia ya mazungumzo kati ya mwajiri na Idara hiyo.

Akifafanua baada kumaliza kikao chake na wawakilishi wa kampuni 30 za kutengeneza dawa kutoka India zinazojiandaa kuwekeza nchini, Balozi Arya alisema baada ya kubaini tatizo kuwa mkanganyiko wa mawasiliano, ndiyo maana wameruhusu kampuni hizo kuwekeza nchini.

“Unajua zipo ajira za muda, zingine miaka miwili, hivyo udhaifu wa mawasiliano ulisababisha sintofahamu, hivyo taratibu za kufanya ukaguzi zinapaswa kuchukuliwa na vibali vitolewe maisha yaendelee,” alisema.

Balozi Arya alisisitiza kuwa jitihada za kumaliza sintofahamu hiyo, zinaendelea kwa njia ya mazungumzo na ofisi yake kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania, watahakikisha suala hilo linamalizika kidiplomasia bila kuathiri ushirikiano uliopo.

Akizungumzia wawekezaji hao kutoka India, Balozi Arya alisema sekta ya viwanda vya dawa India, mwaka jana iliingizia nchi hiyo dola bilioni 16.5 za Marekani sawa na Sh trilioni 36.8 ambayo ni asilimia 50 ya bidhaa zote zilizouzwa nje ya nchi hiyo.

Mkurugenzi wa Uhakiki wa Ubora wa Huduma za Afya nchini kutoka Wizara ya Afya, Dk Mohamed Ally aliyekuwa mgeni rasmi kwenye   mkutano huo, alisema asilimia 80 ya dawa zinazotumika nchini zinatoka nje ya nchi.

Alisema kati ya asilimia hizo, 60 zinanunuliwa India, hivyo ujio wa kampuni hizo ni faraja kwa Tanzania katika kipindi ambacho nchi inatarajia kuingia kwenye uchumi wa viwanda.

“Serikali tumeandaa mazingira mazuri ya uwekezaji, hivyo tumepata fursa ya kushawishi kampuni za dawa kujenga viwanda nchini, ili kurahisisha upatikanaji wake kufikia malengo ya Serikali kununua dawa viwandani,” alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Hiiti Sillo alisema wajibu wake ni kuhakikisha ubora wa chakula na dawa nchini, hivyo  lazima usajili ufanyike kwa ajili ya ukaguzi wa ubora na kulinda usalama.

“Tuko tayari kutoa msaada kwa wawekezaji ambao watahitaji kufahamu taratibu za usajili wa dawa na nyinginezo,” alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bohari ya Dawa (MSD), Laurean Bwanakunu alihakikishia kampuni hizo za dawa kupata soko la bidhaa zao kwa kuwa wajibu wake ni kununua dawa, kuhifadhi na kusambaza.

“Tunawakaribisha kujenga viwanda vya dawa nchini ili kurahisisha upatikanaji wake kwani tunakabiliana na changamoto, tunapoagiza dawa leo tunazipata baada ya miezi sita,” alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo