Wabunge ‘wamtega’ Ndugai


SAKATA LA MAKONDA

Waandishi Wetu

Job Ndugai
SASA ni wazi kuwa Spika Job Ndugai ana kibarua kizito kuhitimisha kwa vitendo utekelezaji wa maazimio manne ya Bunge, likiwemo la kuwaita wateule wawili wa Rais kuwahoji kuhusu matamshi yao dhidi ya mhimili huo wa dola.

Wakati wabunge wamelieleza JAMBO LEO jinsi wanavyosubiri kauli yake kuhitimisha suala hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, George Mkuchika na Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashillilah nao wamemtupia mpira Spika kuhusu suala hilo.

Jumamosi iliyopita Ndugai aliliambia JAMBO LEO kuwa mwenye mamlaka ya kutoa barua ya wito kwa wateule hao ambao ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti ni Dk. Kashillilah ambaye jana alisema jukumu hilo lipo chini ya Spika.

Kabla ya kauli hiyo, Ndugai alinukuliwa na gazeti hili Jumatano iliyopita  akisema kuwa anashughulikia jambo hilo na likikamilika atavitaarifu vyombo vya habari.

Sakata la Makonda na Mnyeti liliibuka katika Mkutano wa Sita wa Bunge uliomaliza Februari 10 mwaka huu mjini Dodoma, baada ya mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara kutoa hoja kwamba wateule hao walitoa matamshi yanayoingilia haki na madaraka ya Bunge.

Katika hoja hiyo, Waitara alisema Makonda alisema wabunge huwa wanakwenda bungeni kusinzia, kauli ambayo inakiuka haki za Bunge na kwamba Mnyeti alitumia mitandao ya kijamii kuwaita wabunge  wapuuzi.

Akitangaza maazimio hayo baada ya kupitishwa na wabunge, Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge alisema wateule hao wataitwa kujieleza mbele ya kamati ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.

“Kamati yetu inafanya kazi kwa maelekezo ya Spika. Tukipokea maagizo ndio tutakutana na kujadili, “ alisema Mkuchika.
Wakati Mkuchika akieleza hayo, Dk Kashillilah alisema, “Unataka kufahamu hilo jambo kupitia kwangu? Hayo mambo muulizeni Spika siyo yangu.”

Licha ya juhudi za kumtafuta Ndugai jana kugonga mwamba kutokana na simu yake kuita bila majibu, wabunge mbalimbali walionesha imani kwa Spika huyo na kusisitiza kuwa yeye ndio mwenye jukumu la mwisho katika utekelezaji wa maazimio hayo.

Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Suzan Lyimo alisema baada ya maazimio ambayo wabunge wote waliyapitisha,  lilikuwa ni jukumu la Katibu wa Bunge na Spika kupeleka barua za wito kwa wahusika.

“Siyo kwamba maazimio yale yalipofikiwa basi wahusika wanapaswa kufika na kujieleza bali inahitaji muda wa kuitwa lakini pia kukutana kwa kamati ambayo ina wajumbe 18. Wajumbe hawa wanahitaji kupewa posho kutokana na muda ambao watautumia kuendesha vikao vyao,” alisema Lyimo ambaye ni mjumbe wa kamati hiyo.

“Kamati yetu ni tofauti na kamati nyingine. Sisi tunakutana kwa dharura, inawezekana wahusika wameshapelekewa barua ya wito lakini Spika kwa busara zake akaona asubiri vikao vya kamati vikianza ndio iunganishwe moja kwa moja kwa kukwepa gharama za matumizi.”

Kauli hiyo iliungwa mkono na Mbunge wa Vwawa (CCM) Joseph Hasunga na kwenda mbali zaidi kuwa wabunge sasa wapo katika majimbo yao na huenda Spika amelisitisha jambo hilo mpaka vitakapoanza vikao vya kamati.

“Maazimio yakitolewa yanaenda moja kwa moja serikalini hivyo ni lazima waitwe haiwezi kupingika. Tusiwe na hofu muda bado upo na vikao vya kamati vinaanza mwanzoni mwa mwezi ujao, nadhani tutapata mrejesho,” alisema Hasunga.

Mbunge wa Mkuranga (CCM), Abdallah Ulega alisema Ndugai hawezi kwenda kinyume na maazimio hayo na kusisitiza kuwa ili wateule hao wa Rais wahojiwe, ni lazima taratibu zifuatwe.

“Siyo kwamba baada ya maazimio basi nao wanakwenda bungeni. Bunge lina taratibu zake kila kitu kipo kwa Spika yeye ndio anatakiwa aite kamati yake ili  wawajadili lakini nafikiri anasubiri vikao vya jumla vya kamati,” alisema.

“Usidhani suala hili limekwisha unapaswa kutambua kuwa Bunge likishaamuru kitu kifanyike hakuna chombo kingine chenye uwezo wa kupinga ikiwemo Rais.  Hili suala lipo chini ya Spika yeye ndio anatakiwa ampe oda Katibu wa Bunge,” alisema Khatib Said haji, mbunge wa Konde (CUF).

“Tusubiri tuone kamati zikianza. Spika hawezi kupingana na wabunge wake na ninafahamu ameshaanza kuchukua hatua dhidi ya suala hili hivyo hakuna mabadiliko yoyote.”

Maazimio mengine
Maazimio mengine yaliyopitishwa na Bunge ni endapo kamati itaridhika kwamba kuna jinai, Mwanasheria Mkuu wa Serikali awasiliane na vyombo vingine vya kiuchunguzi kufuatilia suala hilo na kuchukua hatua kwa taratibu za vyombo hivyo.

Vilevuile, Bunge liliazimia kwa kauli moja kuwa Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), atume waraka kwa wakuu wa mikoa na wilayta kutoingilia mhimili wa Bunge.

Katika azimio jingine, endapo kamati hiyo ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge itathibitisha tuhuma dhidi yao, Bunge linaazimia mamlaka ya uteuzi ijulishwe ili kuwawajibisha.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo