Wahariri wahimizwa kuibua fursa za kilimo SAGCOT


Mwandishi Wetu

Viongozi wa Jukwaa la Wahariri
KITUO cha Mpango wa Kuendeleza Kilimo Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), kimewataka wahariri kuwa mstari wa mbele kuhamasisha kilimo na kutangaza fursa zilizopo kwenye sekta hiyo.

Rai hiyo ilitolewa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa SAGCOT, Geoffrey Kirenga wakati akizungumza kwenye semina iliyoandaliwa mwisho mwa wiki kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kuwaeleza wanahabari shughuli zinachofanywa na kituo hicho katika kuinua kipato cha wakulima wadogo.

“Katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati, Tanzania ina fursa nyingi za kilimo lakini hazijafikiwa au kuchangamkiwa kutokana na kukosa uthubutu,” alisema.

Kirenga aliongeza kuwa, “wanahabari mna nafasi nzuri kuzitangaza fursa hizo kwa Watanzania kwa kutumia vyombo vyenu na kuhakikisha sekta ya kilimo nchini inakua na kuinua kipato cha wakulima wadogo,”.

Alisema sekta ya kilimo ina fursa nyingi kwa maendeleo ya Watanzania na Taifa kwa jumla huku akitoa mwito kwa wanahabari kuandika zaidi habari zinazohusu sekta ya kilimo na fursa zake ili kuhamasisha Watanzania wengi kujikita katika sekta hiyo.

Akitolea mfano kiwanda cha kukoboa mpunga kilichopo Kilombero, alisema ni cha kwanza kwa ukubwa na ubora katika ukanda huu.

“ASAS ni kiwanda kinachoongoza kwa usindikazi maziwa katika ukanda huu kwa siku kina uwezo wa kusindika lita 50,000 lakini wanapata lita 20,000 tu kutoka kwa wafugaji,” alisema.

Alisema fursa hizo zinapotea na sababu kubwa ni ng’ombe kukosa malisho bora na cha kushangaza Australia wanatumia nyasi za Tanzania kulisha ng’ombe wao halafu wanakuja kutuuzia nyama na maziwa.

“Vilevile tuna tatizo la kuhifadhi chakula, mahindi yanayozalishwa nchini kwa mwaka ni kati ya tani milioni sita hadi saba lakini yanayohifadhiwa kwa njia za kisasa ni kati ya tani milioni moja hadi mbili, yaliyobaki yanahifadhiwa kwa njia za kienyeji yanaishia kuharibika, ipo haja serikali ikatengeneza maghala katika maeneo ya uzalishaji,” alisema Kirenga.

Akizungumzia malengo ya kuanzishwa mpango huo, Naibu Ofisa Mtendaji Mkuu wa SAGCOT, Jennifer Baarn alisema, “kazi yetu ni kama madalali baina ya wakulima na serikali, tunaangalia matatizo yanayorudisha nyuma sekta ya kilimo na kwa pamoja tunatafuta namna ya kuyatatua. Lengo ni kuhakikisha mnyororo wa kuongeza thamani ya mazao unaleta tija kwa wakulima hasa wadogo.”

Alisema wamejiwekea utaratibu ambapo kila mwaka kunafanyika kongamano linalowakutanisha wadau wa kilimo ambao kwa pamoja wanajadili njia sahihi za kufanikisha baadhi ya maazimio yaliyofikiwa mwaka uliopita.

Naibu Ofisa huyo alisema kwa mwaka huu kongamano hilo litafanyika mapema mwezi ujao jijini Dar es Salaam.

Miongoni mwa wahariri waliohudhuria semina hiyo kutoka gazeti la Raia Mwema, Ezekiel Kamwaga alisema kwa sasa ipo haja wananchi wakaelewa kuhusiana na kilimo kwa sababu shughuli hiyo ina kipato kikubwa.

“Yapo mengi niliyojifunza kwa hakika kilimo kinalipa, kazi yetu wanahabari ni kuieleza jamii umuhimu wa kilimo na kazi hiyo tutaifanya kwa                weledi,” alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo