Pombe ya ‘viroba’ mwisho Machi mosi


Mwandishi Wetu

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuanzia Machi mosi, Serikali itapiga marufuku matumizi ya pakiti za plastiki kufungashia pombe kali maarufu kwa jina la ‘viroba’.

“Tumekaa na wenye viwanda na kukubaliana kuwa wanaotengeneza pombe waziweke kwenye ukubwa unaokubalika.

“Sasa hivi viroba vimeenea kila kona hata watoto wa shule za msingi wanatumia kwa sababu ni rahisi kuweka mfukoni na kutembea navyo. Kuanzia tarehe moja Machi, tutakayemkamata ameshika pombe ya viroba, sisi na yeye,” alionya.

Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo juzi jioni wakati akizumgumza na maelfu ya wakazi wa mji mdogo wa Mirerani, wilayani Simanjiro akiwa katika siku ya pili ya ziara yake mkoani Manyara.

Alisema agizo hilo linakwenda sambamba na vita dhidi ya dawa za kulevya, kwani mji wa Mirerani unaongoza kwa matumizi ya dawa hizo haramu.

 “Tutawakamata wanaosambaza, wanaouza na wanaokula. Hapa Mirerani kuna bangi, kuna mirungi, kokeni na heroin. Mkuu wa Mkoa hapa panahitaji operesheni kupambana na dawa za kulevya. Piteni kwenye vijiwe na kukagua wanaolegealegea, kisha tuwapime,” alisisitiza.

Akifafanua kuhusu uwekezaji kwenye eneo la Shambalai kutokana na ujumbe ulioandikwa kwenye mabango, Waziri Mkuu alisema katika eneo hilo zimetengwa ekari 500 kwa ajili ya EPZA ili kujenga miundombinu.

“Hilo eneo ni la uwekezaji kwa ajili ya ujenzi wa viwanda, masoko na maduka makubwa. Sote tunafahamu, kuwa Tanzania hivi sasa inaweka msisitizo juu ya ujenzi wa viwanda.

“Pale tunataka tuwe na viwanda vya nyama, vya kushona nguo na kuchakata madini ya tanzanite ili kuyaongeza thamani,” alisema huku akishangiliwa.

Alisema kama kuna mtu ana uhakika kuwa nyumba yake bado haijalipwa fidia eneo lile, akaonane na Mkuu wa Mkoa, Dk Joel Bendera lakini taarifa alizopewa ni kwamba hakuna mtu ambaye hajalipwa.

Waziri Mkuu pia aliwaita wakurugenzi wa kampuni ya TanzaniteOne wampe taarifa ya malalamiko ya wafanyakazi wa kampuni hiyo kwamba hali ilikuwa nafuu wakati kampuni hiyo ikimilikiwa na Wazungu kuliko sasa.

“Nikimaliza ziara ya mkoa huu, nataka Februari 27, wakuu wa hii kampuni waje ofisini kwangu na taarifa kuhusu shughuli za uendeshaji wa madini. Nitawashirikisha wabunge wenu ili waje waseme kwa nini Mzungu ni bora kuliko Mtanzania,” alisema.

“Serikali hii inatarajia kuona Watanzania wakinufaika na rasilimali zao. Haiwezekani tukahimiza uwekezaji wa ndani halafu leo anasifiwa Mzungu kuliko mzawa,” alisema.

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo