Wanne wafa kwa kufukiwa na kifusi mgodini


Moses Ng’wat, Mbeya


WATU wanne wamepoteza maisha na wengine saba wamejeruhiwa, baada ya kufunikwa na kifusi wakati wakichimba dhahabu kwenye mgodi usio rasmi katika kijiji cha Matundasi wilayani Chunya.

Ajali hiyo imetokea juzi saa 4 asubuhi, baada ya watu hao wanaodaiwa kuwa wavamizi, kuanza shughuli za uchimbaji katika mgodi huo ambao hata hivyo mmiliki wake hajafahamika.

Akizungumza kwa njia ya simu jana, Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Rehema Madusa, alithibitisha kutokea kwa maafa hayo na kueleza, miili ya watu hao imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Chunya na majeruhi wanaendelea kupatiwa matibabu hospitalini hapo.

Mkuu huyo wa Wilaya aliwataja waliopoteza maisha kuwa ni Simon Majaliwa (25), mkazi wa kijiji cha Itumpi; Mazoea Mahona (25), mkazi wa Tabora; Benny Bahati (23), mkazi wa Mapogolo na James Alinanuswe (26) mkazi wa Tukuyu, wilayani Rungwe.

Waliojeruhiwa ni Adrew Paul (26), Marco Frederck (22) na Isack James (30) wote wakazi wa kijiji cha Itumpi na Hamis Mwalyosi (25), mkazi wa Mapogolo.

Mkuu huyo wa Wilaya alisema watu wengine watatu hawajafahamika mara moja, kwani baada ya kuokolewa walitokomea kusikojulikana na vyombo vya dola havikufanikiwa kupata maelezo yao.

Kutokana na hali hiyo, Mkuu huyo wa Wilaya ametoa mwito kwa watu wanaojihusisha na uchimbaji madini, kuchukua hadhari hususani wakati huu mvua kubwa zinapoendelea kunyesha.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo