Masogange, Wema uso kwa uso mahakamani


Grace Gurisha

WASANII Wema Sepetu na Agnes Waya maarufu (Masogange) jana walikutana uso kwa uso katika Mahakama ya Kisutu Dar es Salaam, huku kila mmoja akikabiliwa na kesi yake lakini zote zinahusu tuhuma za kutumia dawa za kulevya.

Wema ambaye ni muigizaji wa filamu na Masogange, mnenguaji licha ya kukutana kwa kesi zao, pia familia zao zilikutana zikifuatilia mashtaka dhidi ya ndugu zao huku zikitajwa kuwa na uhasimu.

Wakati Wema akipanda ngazi za mahakama hiyo kwenda kizimbani kwa ajili ya kusikiliza kesi yake kwa mara ya pili, Masogange alikuwa akifikishwa mahakamani hapo chini ya ulinzi wa askari mmoja wa kike.

Katika mahakama hiyo, Masogange (28), amepandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza akishtakiwa kwa mashtaka mawili ya kutumia dawa za kulevya aina ya Heroin na Oxazepam.

Hata hivyo, Masogange alipata dhamana baada ya kusota mahabusu siku nane wakati Jeshi na Polisi lilipomshikilia kwa mahojiano ya tuhuma ya kujihusisha na dawa za kulevya.

Akisoma hati ya mashtaka, Wakili wa Serikali Constantine Kakula alidai jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu kuwa kati ya Februari 7 na 14, 2017 katika maeneo yasiyojulikana ndani ya jiji la Dar es Salaam alitumia dawa za kulevya aina ya Heroin.

Katika shtaka la pili, Kakula alidai kuwa kati ya Februari 7 na 14, 2017 alitumia dawa za kulevya aina ya Oxazepam, ambapo alifanya makosa hayo chini ya kifungu cha 18 (a) cha sheria ya kupambana na dawa za kulevya namba 5 ya mwaka 2015.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Masogange alikana kuhusika na tuhuma hizo na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa ili kuangalia kama upelelezi umekamilika au la.

Hakimu Mashauri alisema ili mshtakiwa awe nje kwa dhamana anatakiwa awe na wadhamini wawili wanaoaminika ambao kila mmoja atasaini bondi ya Sh milioni 10 na mshtakiwa asitoke nje ya jiji la Dar es Salaam bila ya kuwa na kibali cha mahakama.

Hata hivyo, Masogange alikamilisha masharti hao na kuachiwa kwa dhamana na kesi imeahirishwa hadi Machi 21,2017 kwa ajili ya kutajwa ili kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika ama la.

Wema anashtakiwa kwa tuhuma za kukutwa na msokoto mmoja wa bangi na vipande viwili vidogo vya bangi vyenye uzito wa gramu 1.08.

Wakili wa Serikali, Kakula alidai jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 15 mwaka huu kwa kutajwa.

Mbali na Wema washitakiwa wengine ni wafanyakazi wake wa ndani Angelina Msigwa (21) na Matrida Abas (16), ambapo wote wanashitakiwa kwa kosa moja la kukutwa na kiasi kidogo cha dawa za kulevya.

Ilidaiwa kuwa Wema na wenzake walitenda kosa hilo Februari 4, 2017 February mwaka huu, huko nyumbani kwao Kunduchi Ununio Wilaya ya Kinondoni Mkoa wa Dar es Salaam walikutwa na misokoto hiyo.

Baada ya kusomewa shitaka hilo, walikana kuhusika na tuhuma hizo. Hakimu Simba alisema ili washitakiwa wawe nje kwa dhamana wanatakiwa wawe na wadhamini wawili kila mmoja watakaosaini bondi ya Sh milioni tano kwa kila mmoja.

Hata hivyo,Wema na wenzake walitimiza masharti hayo na kuachiwa kwa dhamana, lakini kabla hawajatoka mahakamani Simba aliwataka wahakikishe wasiruke dhamana pindi wanapotakiwa kufika mahakamani wafike.

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo