Jalada kesi ya Jamii Forum layeyuka mahakamani



Grace Gurisha

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, imeshindwa kutoa hukumu ya kesi ya Kikatiba iliyofunguliwa na Kampuni ya Jamii Media ambayo ni wamiliki na waendeshaji wa mitandao ya Jamii Forums na FikraPevu kwa sababu jalada la kesi hiyo halijulikani lilipo.

Wakili wa Kampuni hiyo, Bernedict Alex alisema jana nje ya mahakama hiyo kuwa kutokana na rekodi za mahakama faili hiyo halikuonekana hivyo imeshindwa kutoa hukumu.

Alisema walikwenda kwa karani ambaye ndiye anayehusika na kesi hiyo na kulitafuta jalada la kesi hiyo bila mafanikio, wakaendelea kufuatilia na kubaini kuwa mmoja wa jopo la majaji wa tatu, Jaji Winfrida Koroso amehamishiwa katika Mahakama ya Kifisadi.

“Tumekubaliana na mawakili wa Serikali kulifuatilia suala hili ili tujue mwafaka wa kesi yetu,”alisema Wakili Alex. Kesi hiyo ilikuwa inasikilizwa na Koroso, Jaji Isaya Arufani na Jaji Ignus Kitusi.

Jamii Media waliamua kufungua kesi hiyo kutaka kifungu cha 32 na 38 cha sheria ya Makosa ya Mtandao viangaliwe upya kwani vinasababisha kuvunjwa kwa haki za msingi za Watanzania watumiao mitandao.

Pia, walifungua kupinga amri waliyopewa na polisi ya kutoa taarifa binafsi za wanachama wao dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Jeshi la Polisi Awali, Wakili wa Jamii Media, Shukuru Mkwafu alisema ili kulinda masilahi ya umma, lazima vifungu 26(2) na 30(3) vya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania vizingatiwe.

Alisema Sheria ya Makosa ya Mtandao Namba 14 ya mwaka 2015, inakiuka haki ya kikatiba namba 16 inayoruhusu kuwapo na hali ya faragha na kifungu namba 18 kinazungumzia uhuru wa kujieleza.

Mkwafu alisema baadhi ya vifungu vya sheria ya kimtandao vinakiuka masharti ambayo yamewekwa na katiba hasahasa vinaingilia haki ya faragha ambayo wateja wetu wanayo kikatiba, kwa hiyo wanaiomba mahakama ibatilishe na itamke kuwa vifungu hivyo ni batili kwa kuwa vinaenda kinyume na ibara 16 na 18 ya katiba.

Hatua hiyo ya kufungua shauri Mahakamani imekuja baada ya kuwepo na shinikizo kutoka Jeshi la polisi kumtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Maxence Melo kutoa taarifa za baadhi ya wateja wake.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo