Bodi ya Mikopo yakusanya bilioni 8/-


Salha Mohamed

BODI ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) imekusanya Sh bilioni 8 kati ya Januari hadi sasa kutoka kwa wanufaika wa mikopo yake.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo, Abdulrazaq Badru alibainisha hayo jana alipozungumza na mwandishi wa habari hizi Dar es Salaam.

Alisema ongezeko hilo lilitokana na ziara kwenye kampuni na mashirika yenye wanufaika wa mikopo na kutoa ufafanuzi wa namna ya kulipa fedha hizo.

“Fedha zote si tu zinatoka kwa wadaiwa sugu bali kwa wanufaika wote na kipato kinapanda tofauti na Novemba hadi Desemba ambacho kilikuwa Sh bilioni 6,” alisema.

Alisema ziara waliyofanya imeongeza ari ya kulipa kwa kuwapa waajiri kiwango kipya cha asilimia ya kulipa ambacho ni 15% badala ya 8%.

Badru alisema kiwango hicho kilichoanza kutolewa Januari ni tofauti na kilichoelezwa awali cha asilimia nane.

“Pia tumehakikisha wanakatwa makato yao kwa njia sahihi na waajiri wengi wameitikia mwito kwani walikuwa hawajui kiasi cha kukata na wajibu wao kama waajiri,” alisema.

Alisema mwajiri alipaswa kujua na kutambua mtu anapaswa kutoa taarifa zake kama alikopa, hivyo waliwafanyia wepesi wa kulipa madeni yao.

Aliongeza kwamba wanaendelea kuwatafuta huku akiwataka kujitokeza ili kulipa na kukwepa mkono wa sharia.  

“Nia yetu si kupelekana mahakamani, lakini kulipwa ili wengine wanufaike na mkopo, kwani wako wengi wanahitaji, karibu wote tunaowapata wanalipa,” alisema.

Alisema wale ambao bado Bodi haijawafikia wajitokeze kulipa, huku akibainisha kuwa hadi sasa wadaiwa hao wamepungua kutoka 84,000 hadi 72,000.

“Tumejiwekea lengo hadi Juni, tuwe tumewaondolea watu wote usugu, huku tukiendelea na mikakati ya siku zote kwa kutembelea waajiri na kuhakikisha wanakatwa wanufaika na kuwasilisha,” alisema.

Alisema wataanza awamu ya pili ya kutoa elimu kwa wanufaika na waajiri, ili kuelewa umuhimu wa kulipa fedha hizo na kusaidia wengine ili kuongeza Mfuko wao.

Alisema utaratibu wa kutoa picha za wadaiwa hao bado uko pale pale, kwani kuna taratibu chache wanatarajia kumaliza hivi karibuni.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo