Wahamiaji haramu 25 wa Ethiopia wanaswa


Mashaka Kinaya, Tanga 

Kamanda Benedict Wakulyamba
WAHAMIAJI haramu 25 raia wa Ethiopia wamekamatwa na Polisi wilayani hapa, wakati wakiwa kwenye magari wakisafirishwa kutoka Tarakea, Kilimanjaro kupitia Korogwe hadi Mbeya, lengo likiwa ni kwenda Afrika Kusini.

Taarifa zilieleza, kuwa Waethiopia hao walikamatwa juzi saa 11 jioni eneo la Kiloza, Magila Gereza, wakisafiri kwa magari mawili aina ya Toyota Land Cruiser.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Benedict Wakulyamba, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari, huku akibainisha kuwa wahamiaji hao wanatarajiwa kukabidhiwa kwa Idara ya Uhamiaji ili taratibu zingine za kisheria ziendelee.

Waethiopia hao walikuwa wakitoka Tarakea, Kilimanjaro kupitia Korogwe lengo likiwa kufika Mbeya ili kuendelea na safari yao kwenda Afrika Kusini.

Pamoja na wageni hao kukamatwa, pia madereva Watanzania Mkwawa Emily (40), David Meshack (36) na utingo Nelson Joseph (36) wote walishikiliwa kwa muda Polisi Korogwe kwa mahojiano kabla ya kuletwa mjini hapa kwa taratibu za kisheria.

Magari yaliyohusishwa na tukio hilo ni aina ya Toyota Land Cruiser namba T 892 ASH likiendeshwa na Emily na utingo Joseph lililokuwa na Waethiopia 11 na lililokuwa likiendeshwa na Meshack namba T 646 CKS likiwa na wahamiaji 14.

Wahamiaji hao na umri wao kwenye mabano ni Almayu Kudra (22), Beranu Tudasa (20), Mulegat Yufuma (29), Eyasu Damasha (23), Mulak Morau (26), Feker Mator (26), Eyasu Turfa (25),Takatal Wudal (27), Salum Marekue (25), Tomoroa Bagojam (20), Avinto Tuwili (19) na Hajira Ibrahim (20).

Wengine ni Malya Tala (20), Zayne Ketbo (22), Masfn Zamde (22), Abrmi Digamo (25), Milatu Bachar (21), Lomibise Bolol (22), Lama Loba (24), Ababa Tamile (26), Tamilat Hylee (26), Basmi Fonte (32), Tigante Ababa (15), Dassan Tumiso (18) na Labi Lode (18).

Kukamatwa kwa wageni hao kulimfanya Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Robert Gabriel kusema kuwa ipo haja kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano wa hali na mali kwa vyombo vya ulinzi na usalama.

Gabriel alisema wananchi wanapomhisi au kumtilia shaka mtu kwenye eneo lao kuwa si mwenyeji waitaarifu Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama hatua ambayo itawezesha wahusika kukamatwa kwa mahojiano, huku hatua stahiki zikichukuliwa.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo