Profesa Anna Tibaijuka: Magufuli kinara wa kutetea wajane



Mashaka Mgeta

Profesa Anna Tibaijuka
MIONGONI mwa walioguswa na tukio la Rais John Magufuli kumsikiliza mjane, Swahaba Shosi, aliposhiriki kuhutubia Siku ya Sheria Februari 2, mwaka huu jijini Dar es Salaam ni Mbunge wa Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka.

Rais Magufuli, baada ya kuhutubia hadhira iliyoandaliwa na kuwashirikisha majaji, akajitokeza Shosi akielezea kuchoshwa na namna watendaji wasiokuwa waadilifu katika taasisi tofauti za umma ikiwamo Mahakama, wanavyopanga kumdhulumu haki ya kurithi mali za marehemu mume wake.

Baada ya kumsikiliza akijieleza kwa ujasiri, licha ya majonzi yaliyomsababisha kutoa machozi takribani wakati wote alipojieleza, Rais Magufuli aliamuru suala hilo lishughulikiwe haraka huku Shosi akipewa ulinzi na jeshi la polisi.

Tukio hilo liligusa hisia za watu kwa namna tofauti, wengi wao kupitia mijadala kwenye mitandao ya kijamii, wakimpongeza Rais Magufuli kwa hatua hiyo.

Katikati ya hali hiyo, anajitokeza Profesa Tibaijuka, akisema kadhia inayomkabili Shosi ni sawa na ile aliyokutana nayo, ikihusu ardhi iliyoachwa na marehemu mume wake, lakini ikageuzwa na kufanywa hila aonekane kuwa ni mporaji.

Lakini Tibaijuka kupitia waraka wake anasema, ni Rais Magufuli alipofanya ziara mkoani Kagera hivi karibuni, kulitolewa taarifa za uongozi dhidi yake (Profesa Tibaijuka) ambazo hata hivyo, mwitikio wake (Rais Magufuli) ukawa mwenye kumsaidia dhidi ya wabaya wake.

Waraka wa Profesa Tibaijuka uliandikwa hivi:- Wanawake hatuna budi kumshukuru na kumpongeza Rais Magufuli kwa kututetea sisi wajane tunaonyanyaswa na mifumo dume na kuporwa haki zetu na watoto wetu.

Jana (Februari 2, mwaka huu) Rais alitenda makuu kuagiza kwamba yule mama aliyekuwa ameonewa na kuhangaishwa kwa muda mrefu, sio tu kesi yake isikilizwe lakini pia apewe ulinzi wa polisi.

Kwa kumbukumbu zangu, hii haijawahi kutokea kwa mnyonge aliyekata kamba za ulinzi mkali unaomzunguka Rais badala ya kwenda rumande, kupewa ulinzi wa polisi yeye mwenyewe. Hili linathibitisha kauli ya mara kwa mara ya Rais Magufuli kwamba “msema kweli ni mpenzi wa Mungu”.

Kwa kuwa Rais Magufuli kajitanabaisha na kuudhihirishia umma kuwa anachotaka ni ukweli na uwazi, huyu mama mwenzetu alikuwa na nguvu na imani kwamba akimfikia (Rais Magufuli), matatizo yake yatakwisha.

Atapata kusikilizwa na haki yake ambayo vyombo vya utawala na Mahakama vimeshindwa kumpatia kwa muda mrefu itapatikana. Vyombo hivi hushindwa kwa sababu baadhi ya wahusika wanakuwa na maslahi binafsi katika migogoro kama hiyo.

Wanaichukulia migogoro hiyo kuwa fursa na mtaji wasiopenda uishe. Kwa hiyo anayedai haki yake anawekewa vikwazo na wale waliotarajiwa kumsaidia.Kilio cha yule mama na maelezo yake yalikuwa wazi, kahangaishwa kwa muda mrefu. Alikuwa tayari kujilipua. Ninampongeza mama kwa kutokata tamaa.

Na ninampongeza kwa ujasiri kuja mbele ya Rais Magufuli pamoja na ugumu wa hatua hiyo. Aidha ninamuombea mafanikio kwa hatua zinazofuata. Mungu hujibu uonevu kwa wanaomtumainia.

Katika kujadili suala hili nami sina budi kurejea tukio kama hili mapema Januari 2, mwaka huu, Kyamyorwa mkoa wa Kagera.

Akiwa katika ziara ya kutembelea walioathirika kwa tetemeko mkoani kwetu, Rais Magufuli alinitetea na kuniokoa mikononi mwa watesi wangu wa muda mrefu jimboni mwangu Muleba Kusini.

Kwa sababu za kisiasa, walikuwa wananikashfu kwa kudai nimepora ardhi ya wananchi wakati wao ndio walikuwa wakiwadanganya wananchi wahamiaji kutoka mikoa jirani na kuwatoza fedha kwa kuwadanganya watawagawia shamba langu la urithi kutoka kwa marehemu mume wangu.

Marehemu alimilikishwa shamba hilo kihalali miaka mingi ya nyuma eneo likiwa pori tupu. Watu hao wanajificha nyuma ya pazia la siasa za upinzani na huwa wanawarubuni hata maafisa wa Serikali wasiokuwa waaminifu na wenye tamaa ya ardhi hiyo, kunisumbua.

Rais Magufuli alifika hapo na kuwakuta vijana wa kukodishwa tayari wana mabango ya kunikashfu nimepora ardhi.

Walikuwa wanaongozwa na Diwani (tunahifadhi jina lake kwa vile hakupatikana kuzungumzia tuhuma hiyo) wa Chadema ambaye mtaji wake wa kisiasa ni kunikashfu, akishirikiana na wabaya wengine ngazi za juu. Awali genge hilo kama kawaida yao walisha waandaa vijana wa kunizomea Rais Magufuli aliposimama Muleba Mjini.

Waliamini mara baada ya kushuhudia zomeazomea, Rais Magufuli akifika Kyamyorwa kwenye shamba langu na kukutana na mabango na kelele dhidi yangu, ataninyang’anya shamba ili kuwafurahisha wananchi hao. Wengine wala hawakuwa wenyeji bali walikuwa wamesombwa kutoka mbali.

Videdea vya pikipiki kutoka Kyamyorwa kuelekea Muleba Mjini vilikuwa tayari. Mgeni rasmi kupokea maandamano hayo (jina linahifadhiwa) tayari alikuwa Muleba akisubiri.

Lakini tofauti na mategemeo yao, Rais Magufuli msema kweli na mpenzi wa Mungu na mtoa haki hakufurahishwa na mpango wao huo mwovu. Aliwaonya watu wa Muleba kwamba wajitafakari ni wa aina gani. Rais alisema kabla ya kuondoka kuelekea Kyamyorwa ambayo ni jirani na nyumbani kwake Chato.

Yaliyojiri Kyamyorwa taifa lote limeshuhudia. Rais Magufuli aliwashushua waliokuwa wamepanga kupora ardhi yangu na katika kufanya hivyo, kunigeuza mimi mhanga ndiye mkosaji. Rais Magufuli alieleza ukweli wa ardhi hiyo aliyowahi kuifanyia kazi alipokuwa Waziri wa Ardhi.

Shamba limeendelezwa kwa kilimo cha mbegu bora, mifugo na uhifadhi wa mazingira na linalipiwa kodi ya ardhi kila mwaka. Shamba lina hati ya miaka 99.

Tukio hilo lilinipa faraja kubwa na ninalifananisha kwa namna fulani na tukio la mjane wa jana (Februari 2) au zaidi kwa sababu Rais Magufuli alinitetea pamoja na kwamba sikuwepo katika ziara yake hiyo.

Kwa kuwa sikujua Rais Magufuli angelisimama jimboni kwangu Muleba Mjini, mimi mara baada ya kukamilisha ziara yake Bukoba Mjini niliingia makubaliano na Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako kubaki Bukoba Mjini kumsindikiza Katibu Mkuu Elimu.

Kwa pamoja tulimpeleka Balozi wa Uingereza, Sara Cooke kutembelea Shule ya Sekondari ya Wasichana Rugambwa ambayo nayo imeathirika na tetemeko ili ipewe msaada.

Mimi nilisoma Rugambwa kwa hiyo ni mdau mkubwa. Nikiwa hapo niliweza kumueleza Balozi shule hiyo ilivyokuwa enzi zetu kama juhudi za kuhamasisha msaada wake kwa ukarabati kama alivyotoa kwa sekondari kongwe ya Ihungo.

Kwa hiyo sikuwepo jimboni kwangu wakati wategeshi wa siasa wananihujumu mbele ya Rais wa nchi.

Kwa hiyo kwa msaada mkubwa aliopewa mama (Shosi) na kwangu mie na wengine ambao mambo yao labda hayapo hadharani, ninasema wanawake tujitambue bado tuna safari ndefu.

Haijalishi wewe una elimu, cheo au nafasi gani katika jamii. Mfumo dume unafanya kazi kukudidimiza. Ikitokea Rais aliyeshika usukani si mtu mkweli na mcha Mungu na mtu wa haki, mwanamke utakuwa wa kwanza kulaumiwa, kuonewa na kutolewa kafara.

Kwa mantiki hiyo wanawake ni wadau wa kwanza katika kuhitaji kiongozi bora. Tunategemea utetezi na ulinzi wake.

Niliwahi kusema na ninarudia tena, kwa kuwa na Rais Magufuli, Tanzania tumejaliwa kupata kiongozi siyo tu Rais, bali kiongozi anapopewa dhana ya Urais anaitumia kama tunavyoona sasa. Kutengeneza upepo sio kuufuata ili kufurahisha mifumo kandamizi kwa kuitolea kafara.

Nimalize makala hii na ombi. Rais Magufuli wanawake wengi tuko nyuma yako. Tatizo la kuwanyonga vikongwe kwa kudai ardhi na haki zao katika jamii huko vijijini bado lipo.

Ninaomba ulitupie jicho jambo hili. Kama ulivyomkabidhi mama mlalamikaji ulinzi wa polisi uwatake wakuu wa wilaya na wakuu wa polisi wa wilaya, kuwalinda vikongwe katika maeneo yao dhidi ya dhuluma na vitendo vya ukatili.

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo