Wachapishaji watakiwa kujiorodhesha


Leonce Zimbandu

Cassian Chibogoyo
OFISI ya Mpigachapa Mkuu wa Serikali imetoa siku 44 kwa wachapishaji nchini kujiorodhesha kwenye ofisi hiyo kabla ya operesheni ya kuwasaka nyumba kwa nyumba kuanza.

Mpigachapa Mkuu wa Serikali, Cassian Chibogoyo, alisema Dar es Salaam jana, kwamba lengo la kuwataka kujiorodhesha ni kuiwezesha Serikali na umma kuwatambua na kujiepusha kujificha iwapo wanatekeleza wajibu wao wa uchapishaji kwa kuzingatia sheria.

Chibogoyo alikuwa akitoa msisitizo wa matumizi sahihi ya vielelezo vya Taifa ambavyo ni Bendera, Nembo na Wimbo wa Taifa.

Alisema katika kuhakikisha suala hilo linafanikiwa, Serikali imeandaa mkakati wa kukabiliana na wachapishaji wa nyaraka bandia hata kama limefanikiwa lakini bado baadhi wanaendelea kukaidi.

“Unajua nyaraka bandia ni janga kwa jamii, hivyo ofisi yangu inawataka wachapishaji kujiorodhesha hadi Machi 30, baadaye tutafuata njia iliyotumiwa na Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma kuhakiki vyeti, nasi tutahakiki wachapishaji na ofisi za Serikali ambazo zimegoma kutundika Bendera ya Taifa nchini,” alisema.

Alisema uchapishaji ni mwito tena una maadili yake, hivyo ni lazima kuzingatia iwapo mchapishaji hawezi kufuata taratibu zilizopo ni busara kutafuta biashara nyingine.

Aidha, Chibogoyo aliwataka vijana wanaokimbiza Mwenge watoe maelezo kuhusu umuhimu wa Mwenge wa Uhuru hasa wakati wa kuzindua miradi nchini.

Alisema maelezo hayo yatasaidia kuondoa sintofahamu kwa watu ambao wanajenga hoja kuwa Mwenge hutumia pesa nyingi bila sababu za msingi.

Alisema ikikumbukwe kuwa Mwenge wa Uhuru ni miongoni mwa nyenzo za kuleta maendeleo ya nchi baada ya kuondoa maadui ujinga, maradhi na umasikini.

Aliongeza kuwa baada ya Mwenge kuwekwa Mlima Kilimanjaro, Watanganyika walijikusanya, kuungana na kupigania haki zao kwa lengo la kujikomboa.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo