Wamshauri JPM kuhusu Watanzania kunyongwa


Charles James

Rais John Magufuli
SIKU moja baada ya Rais John Magufuli kutangaza kuwa Serikali haitatetea Watanzania wanaokamatwa nje ya nchi kwa kufanya biashara ya dawa za kulevya, baadhi ya wasomi na wanasheria wametoa maoni tofauti kuhusu kauli hiyo baadhi wakiipinga wengine wakiunga mkono.

Akizungumza wakati wa kumwapisha Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers Sianga na Kamishna Mkuu wa Uhamiaji, Dk Anna Makakala juzi, Rais Magufuli alisema hakuna Serikali inayoweza kutetea watu wanaojihusisha na biashara hiyo na kumtaka Waziri wa Mambo ya Nje na mabalozi kuwaacha ili wapate haki zao.

Akitoa maoni yake, Mkurugenzi wa Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC), Dk Helen Kijo-Bisimba alisema yawezekana Rais alikuwa na hasira kutokana na kukerwa na namna biashara hiyo inavyoharibu picha ya Tanzania.  

Alisema pamoja na kwamba biashara hiyo ni haramu na imekuwa na athari kubwa kwa nchi ikiwamo kuua nguvukazi ya Taifa ambapo vijana wengi wameathirika, bado kama Rais anapaswa kuhakikisha raia wake hawapati adhabu kubwa ambayo hata nchini haitolewi.

“Siungi mkono kusema kama wananyongwa wanyongwe tu, akumbuke kwamba adhafu ya kifo inakwenda kinyume na sheria ya haki za binadamu ambayo Tanzania iliisaini sasa utaruhusu vipi wananchi wapate adhabu kali ambayo hata nchini haitolewi?

“Nchi zingine husaidia raia wao wanapopatwa na adhabu kali ambayo inakiuka haki za binadamu, ipo kesi miaka ya nyuma ya raia wa Trinad &Tobago ambaye alihukumiwa kunyongwa nchini lakini  Waziri Mkuu wao akaomba wamchukue akaadhibiwe kwao,” alisema Dk Kijo-Bisimba.

Katika kauli yake Rais Magufuli alisema kama mtu ameshikwa katika nchi yoyote ambayo sheria yake ni kunyongwa Serikali itamwacha anyongwe, “nasema hili kwa dhati simung’unyi maneno, kwani tukichekacheka Taifa letu litaangamia.”

Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari ambaye kitaaluma ni Wakili, alisema Rais Magufuli alitoa kauli hiyo bila kujua kwamba kuna nchi ambazo tayari zina makubaliano na Tanzania za kubadilishana wafungwa ili wakahukumiwe kwenye nchi zao.

Profesa Safari alisema kauli hiyo haioneshi kama Rais anajali wananchi wake kwani kitendo cha kusema mabalozi wasishughulike nao ni makosa, kwani inawezekana ipo orodha ya Watanzania ambao wanakamatwa kimakosa na hivyo kukosa msaada wa nchi kuwanusuru.

“Mfano sisi na Mauritius tuna makubaliano ya kubadilishana wafungwa wetu, sasa kama anasema Serikali haitahusika na kukamatwa kwa raia wake, ina maana anatoa uhuru kwa nchi zingine kukiuka makubaliano yetu, hii itasababisha kushuhudia watu wengi wakihukumiwa bila kuhusika kwa sababu Serikali tayari imeshajitoa,” alisema Profesa Safari.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Kitivo cha Sheria, Dk Onesmo Kyauke alisema inawezekana Rais alizungumza hivyo kuonesha msimamo wake wa namna gani anapiga vita dawa za kulevya.

“Ukitazama takwimu za raia wa Tanzania waliokamatwa nje ya nchi wakihusishwa na biashara hii ni kubwa na wengi walikuwa wanapata msaada kutoka balozi zetu, lakini kitendo cha Rais kusema waachwe kitasaidia kwa kiasi fulani kupunguza orodha ya Watanzania wanaojihusisha na ‘unga’ ili kulinda sura ya nchi yetu,” alisema Dk Kyauke.

Rais Magufuli alisema jumla ya Watanzania 1,007 wamekamatwa na kuhukumiwa kunyongwa katika nchi 19 tofauti duniani.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo