Majaliwa aasa mabalozi wa Tanzania


Mwandishi Wetu

Kassim Majaliwa
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ametaka mabalozi wa Tanzania kwenye nchi mbalimbali duniani, kuhakikisha wanatumia uwakilishi wao kutafuta wawekezaji kwenye sekta ya viwanda nchini.

Amesema  mkakati wa Serikali ni kuimarisha uchumi  hadi wa kati kupitia sekta ya viwanda, hivyo jukumu la mabalozi hao ni kuhakikisha jambo hilo linafanikiwa.

Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana, alipokutana na mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi za Uturuki, Brazil, China, Italia, Ufaransa, DR Congo na Uswisi.

Mabalozi hao ni Dk Emmanuel Nchimbi (Brazil), Elizabeth Kiondo (Uturuki), George Madafa (Italia), James Msekela (Uswisi), Samuel Shelukindo (Ufaransa), Paul Mella (DRC), na Mbelwa Kairuki (China).

“Serikali inahitaji watu wa kuja kuwekeza katika viwanda ili kuongeza thamani ya mazao kabla ya kuyauza nje ya nchi, hivyo jukumu lenu ni kuhakikisha tunapata wawekezaji wenye sifa,” amesema.

Pia Waziri Mkuu aliwataka mabalozi hao kutumia uwakilishi wao kwenye nchi hizo kwa kuhakikisha wanatangaza vivutio vya utalii nchini ili kuongeza idadi ya watalii wanaokuja.

“Tulinde bidhaa za ndani ya nchi yetu, mfano madini ya tanzanite ambayo yanazalishwa Tanzania pekee, lakini leo yanasababisha nchi zingine kusifiwa kwa uzalishaji zikiwamo India na China, hivyo jukumu lenu ni kuhakikisha mnatangaza madini yetu ipasavyo,” amesema.

Aidha, Waziri Mkuu aliwataka mabalozi hao kulinda maslahi ya Taifa kwenye nchi hizo ikiwa ni pamoja na kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na mataifa hayo.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwataka mabalozi hao kuwatambua Watanzania wanaoishi kwenye mataifa hayo na kushirikiana nao kutafuta wawekezaji kuwekeza nchini.

Balozi Mella ambaye alizungumza kwa niaba ya mabalozi wenzake, alimhakikishia Waziri Mkuu kwamba watatekeleza wajibu wao ipasavyo.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo