Mahakama yazuia Mbowe kukamatwa


Celina Mathew

Freeman Mbowe
MAHAKAMA Kuu imetoa zuio la muda kukamatwa kwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, hadi shauri lake la msingi katika kesi ya Kikatiba litakaposikilizwa keshokutwa Februari 23.

Februari 10 mwaka huu, Mbowe alifungua kesi ya kikatiba dhidi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salam, Paul Makonda; Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro na Mkuu wa Upelelezi wa Kanda hiyo, Kamilius Wambura.

Akizungumza Dar es Salaam jana nje ya Mahakama Kuu, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, alisema hatua hiyo imetokana na uamuzi uliotolewa na jopo la majaji watatu wa mahakama hiyo, kuhusu agizo la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Makonda.

Alisema mahakama hiyo imeamua wanaotaka kumkamata Mbowe, wazuiliwe hadi shauri la msingi alilofungua litakaposikilizwa.

“Hivyo Mahakama imetoa zuio la muda hadi kesi itakaposikilizwa siku ya Ijumaa saa 7:30 mchana, ikiwa na maana kuwa polisi wamezuiliwa kumkamata Mbowe na Mahakama imesema watakuwa na uwezo wa kumwita kwa mahojiano, kama watataka na si kumkamata,” alisema Lissu akinukuu uamuzi wa majaji hao.

Aliongeza: “Kwa maana hiyo mbinde za kina Sirro zimezuiliwa kwa muda mpaka siku hiyo ya Ijumaa maombi yenyewe yatakaposikilizwa.”

Lissu alisema kuwa Mahakama hiyo pia imetoa ruhusa kwa mleta maombi (Mbowe), kurekebisha maombi aliyopeleka mahakamani, ili kumjumuisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kwenye mashauri hayo na kufanya marekebisho mengine madogo yanayofaa kwenye shauri hilo.

Mahakama imeamua marekebisho yafanywe hadi kufikia Februari 27 mwaka huu na yatajibiwa baada ya Machi 6, ndipo watakutana tena mahakamani hapo Machi 8 mwaka huu saa 8:00 mchana,” alisema Mwanasheria huyo.

Lissu aliongeza kuwa ugomvi wa zuio hilo, unaendelea Ijumaa mchana na   Mahakama itakuwa ya wazi na si kama ilivyokuwa jana ambapo ilisikilizwa chemba ambako waandishi walizuiliwa kuingia.

Mbowe aliingia mahakamani hapo saa 10:18, akiambatana na baadhi ya viongozi wa Chadema wakiwemo waliotangulia kabla yake, akiwemo Katibu Mkuu, Dk. Vincent Mashinji na Naibu Katibu Mkuu Bara, John Mnyika.

WEngine ni Lissu, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu na wengine na aliondoka 13:14 akiwa na gari yake iliyokuwa imeandikwa KUB ikimaanisha Kiongozi wa Upinzani Bungeni, aina ya Land Cruiser.

Kesi ya Mbowe dhidi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salam, Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, ilisajiliwa kwa jina la Kesi ya Kikatiba namba 1 ya 2017  kwenye Mahakama ya Kuu masijala ya Katiba (Masijala Mkuu).


Kwenye Kesi hiyo, Mbowe aliomba Mahakama Kuu itamke na kuwa Mkuu wa Mkoa hana mmalaka ya kudhalilisha na kukamata.

Mbowe pia aliiomba Mahakama itengue vifungu vya 5&7 vya Sheria ya Tawala za Mitaa, kwakuwa ni batili na vinakiuka haki za kikatiba.

Katika kesi hizo Mbowe aliwakilishwa na mawakili toka Kurugenzi ya Katiba Sheria na Haki za Binadamu ya Chadema.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo