Jecha ‘aahirisha’ kesi ya uchochezi


Grace Gurisha

SWALI kuhusu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha limeilazimisha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kuahirisha kesi ya uchochezi.

Kesi hiyo inawakabili Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na wahariri wa Gazeti la Mawio, baada ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Salum Hamduni kukataa kujibu swali la Lissu lililotaka kujua kama Jecha ana mamlaka ya kufuta Uchaguzi Mkuu au la.

Suali hilo lilizua mvutano mkali wa kisheria, wakati Lissu akijitetea katika kesi ya tuhuma za kuchapisha taarifa za uchochezi yenye kichwa cha habari kisemacho, Machafuko yaja Zanzibar.

Lissu alimtaka Hamduni kujibu swali hilo, kwa sababu hati ya mashitaka inaruhusu swali hilo, hali ambayo ilisababisha mvutano mkali uliosababisha mawakili wa pande zote kuja juu na kuona kila mmoja ana haki kwa kuvutia upande wake.

Lissu alimwambia Hamduni, “shahidi naomba unijibu swali, Jecha ana mamlaka ya kufuta Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar?”

Hamduni alikaa kimya huku Wakili wa Serikali, Paul Kadushi akisimama kupinga swali hilo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

“Hakimu shahidi si mwanasheria wala si mtafsiri wa sheria na wala si mtaalamu wa Katiba ya Zanzibar kwa hiyo napinga  kujibu swali hilo,” alisema Kadushi.

Jibu la Kadushi lilimfanya Lissu apaze sauti kwa kudai kuwa wakili wa Serikali anamlisha maneno ambayo hajayasema na pia anatakiwa ajibu kwa sababu katika hati, mashitaka ya pili yanahusiana na swali alilouliza.

Pia Lissu alikwenda mbali zaidi kwa kumtaka shahidi amweleze kama ilikuwa ni halali yeye kushitakiwa katika kesi hiyo, kutokana na kwamba yeye si mwandishi, mhariri, wala mmiliki wa Mawio wala mchapishaji, lakini shahidi alimjibu kuwa inaweza ikawa halali kutegemea na mazingira.

Lissu hakukubaliana na jibu hilo na kumtaka Kamanda huyo kumweleza ni njia gani ambayo walitumia kula njama ya kutenda kosa hilo, ambapo majibu ya shahidi yalikuwa kwamba hajui ni njia gani walitumia wala wapi walikaa kwa sababu kuna timu ya upelelezi ndiyo ilikuwa inashughulikia suala hilo.

Mbali na Lissu washitakiwa wengine ni Mhariri wa Mawio, Simon Mkina, Jabir Idrisa na  Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob.

Kwa pamoja washitakiwa hao, wanakabiliwa na mashitaka matano likiwamo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.

Inadaiwa kuwa Januari 12 hadi 14, mwaka jana Dar es Salaam, washitakiwa Jabir, Mkina na Lissu, kwa pamoja waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar’.

Katika mashitaka ya pili wanadaiwa kuwa Januari 14, mwaka jana Dar es Salaam,  walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.

Mehboob  anadaiwa kuwa Januari 13, mwaka jana katika jengo la Jamana Ilala,  Dar es Salaam, alichapisha gazeti la Mawio lililokuwa na taarifa za uchochezi.

Alidai mshitakiwa huyo pia alichapisha gazeti hilo bila kuwasilisha hati ya  sheria ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti.

Mbali na mashitaka hayo washitakiwa kwa pamoja wanadaiwa kuwa Januari 14, mwaka jana,  Dar es Salaam, bila mamlaka waliwatisha na kuwatia hofu wananchi wa Zanzibar   wasiweze kuingia kwenye marudio ya Uchaguzi Mkuu.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo