Makonda, Siro waitwa kortini


Grace Gurisha

Paul Makonda
HATUA ya kutaja hadharani majina ya watu wanaodaiwa kutumia na kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya, imechukua sura mpya baada ya Mahakama Kuu nchini kuwaita Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Siro.

Mwingine aliyetakiwa kufika mahakamani hapo leo ni Mkuu wa Upelelezi wa kanda hiyo (ZCO) Kamilius Wambura, huku taarifa zikibainisha kwamba viongozi hao wamepelekewa mwito wa kufika mahakamani hapo kutokana na kesi yaKikatiba iliyofunguliwa dhidi yao na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

Kesi hiyo ya Mbowe ni namba moja ya mwaka 2017, imepangwa kutajwa leo, ambapo pamoja na mambo mengine anapinga mamlaka ya Makonda kumkamata na kudhalilisha watu.

Katika kesi hiyo Mbowe anaiomba Mahakama itamke kuwa vifungu vya Sheria ya Tawala za Mikoa vinavyowapa mamlaka wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kuwakamata watu na kuwatia mbaroni, viko kinyume cha Katiba.

Jopo la majaji watatu litasikiliza kesi hiyo akiwamo, Sekieti Kihiyo (Mwenyekiti wa jopo), Jaji Lugano Mwandambo na Jaji Pellagia Kaday.

Hata hivyo taarifa zaidi zinaeleza kuwa mwito huo wa Mahakama haukupokelewa na Makonda wala Wambura, ikielezwa hawakuwepo ofisini na wasaidizi wao walikataa kusaini ili kuzipokea huku Kamanda Siro akidaiwa kukataa kupokea mwito huo.

Ofisa wa mahakama aliyepeleka mwito huo, Yusuph Juma, baada ya kuelekezwa na Kamanda Sirro kuwa ampelekee mwito huo Wambura, alipokwenda kwa Wambura, hakumkuta.

Kwenye hati hiyo ya mwito kwenda kwa Kamanda Siro, Juma aliandika: “Kwa hiyo wito haujapokelewa.”

Katika hatua nyingine jana Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, alifungua maombi mengine mahakamani hapo akipinga kusudio la Kamanda Siro la kumkamata kama hatajisalimisha katika kituo cha Polisi kwa mahijiano.

Katika maombi hayo namba 21 ya mwaka 2017, Mbowe anaiomba Mahakama iwazuie wadaiwa kutekeleza azma yake ya kumtia mbaroni pamoja na mambo mengine akidai kuwa kuna kesi ya kikatiba ambayo tayari ameifungua mahakani hapo.

Hivyo aliiomba Mahakama itoe amri ya kuwazuia kumkamata hadi hapo kesi hiyo ya kikatiba itakapomalizika na kwamba Mahakama Kuu imwachie na Polisi wasiendelee na mchakato wowote dhidi yake hadi hapo kesi hiyo itakapomalizika.

Katika kesi ya msingi ya Kikatiba, Mbowe anapinga kitendo cha Polisi kumtaka afike kituoni kwa madai kuwa ni utekelezaji wa amri ya Mkuu wa Mkoa.

Alidai kuwa sheria inayompa Mkuu wa Mkoa mamlaka ya kutoa amri ya kumkamata na kumweka ndani mtu, yako kinyume cha Katiba kwa madai kuwa ilitungwa katika mazingira ambayo hapakuwa na vituo vya Polisi vya kutosha.

Hivyo alidai kuwa kwa mazingira ya sasa sheria hiyo imeshapitwa na wakati na anaiomba Mahakama itamke kuwa ni kinyume cha Katiba.

Hata hivyo alisema kuwa hata kama Mkuu wa Mkoa alikuwa anatekeleza mamlaka yake kwa mujibu wa sheria hiyo, basi hakutimiza matakwa ya kisheria, ambayo ni pamoja na kutoa taarifa kwa Hakimu wa Mahakama ya Wilaya au ya Hakimu Mkazi.

Hivyo aliiomba Mahakama kama itaona kuwa Mkuu wa Mkoa alikuwa sawa kutoa amri hiyo, basi imwamuru afuate matakwa ya kisheria, ikiawa ni pamoja na kulinda haki za binadamu katika kutekeleza madaraka yake hayo.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo