Wema, wenzake 11 kizimbani leo


*Ni kwa tuhuma za kujihusisha na mihadarati

*Operesheni ndani ya familia na kaya kuanza  

Hussein Ndubikile

Wema Sepetu kituo cha Polisi cha Kati
MSANII wa maigizo, Wema Sepetu (28) na wengine 11 wanatarajiwa kufikishwa mahakamani leo kwa tuhuma mbalimbali za matumizi ya dawa za kulevya.

Mbali na Wema aliyekuwa Mnyange wa Tanzania mwaka 2006, watuhumiwa wengine ni Hamidu Chambuso, Rajab Salum, Romeo George, Khalid Mohamed ‘TID’, Lulu Shilengwa, Said Masoud na Nassoro Nassoro.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Simon Sirro alisema baada ya kuwahoji, 11 walikiri kujihusisha na dawa hizo huku akieleza kuwa Wema na Omari Micheni(32) walikana ndipo polisi walipowafanyia upekuzi wanakoishi na kuwakuta na misokoto ya bangi.

“Tunaendelea vizuri na opereshani ya kupambana na dawa za kulevya, ndani ya siku tatu tumekamata kete 299 bado hazijathibitika ni dawa za aina gani mpaka zitakapopelekwa kwa Mkemia Mkuu,” alisema.

Alisema baada ya kuwapekua Wema na Omari walikutwa na misokoto hiyo huku mwenzake alikutwa na kete tano za bangi na kwamba wasanii hao wataandaliwa mashitaka na kupelekwa mahakamani.
Hata hivyo, Sirro alisema watuhumiwa hao 11 watafilishwa kiapo baada ya kukiri kutumia dawa hizo.  

Kamanda Sirro alisema hakuna mtuhumiwa aliyeonewa kwani yeye ndiye alichukua jukumu la kuwahoji na watuhumiwa walikiri kutumia dawa za aina ya heroine, bangi na kokeini, hivyo kusaidia kutaja watu wanaowauzia.

Aliongeza kuwa watuhumiwa waliokiri watafikishwa mahakamani kula kiapo kitakachoombwa na Polisi ambacho kitawaweka chini ya uangalizi wa Polisi kwa miaka miwili wakitakiwa kuripoti mara mbili kwa mwezi na kuahidi kuacha tabia hiyo.

Pia alisema polisi walikamata puli ya misokoto mikubwa 104 na kete 107 za bangi.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametoa siku 10 kwa wenyeviti wa Mitaa kutoa taarifa za nyendo za wanaojihusisha na matumizi na biashara ya mihadarati.

Ameonya kuwa wasipofanya hivyo wataunganishwa kwenye kesi za watuhumiwa watakaokamatwa kwenye mitaa yao.

Mkuu wa Mkoa pia  alitoa siku 10 kwa wazazi na walezi kutoa taarifa kwenye madawati ya upelelezi, za watoto wao endapo wanajihusisha na dawa hizo.

Aliwataka wanaotumia na wanaofanya biashara ya dawa hizo wajisalimishe Polisi kabla hawajachukuliwa hatua za kisheria.

Aliitaka jamii kutambua kuwa Rais John Magufuli hataki kusikia biashara na matumizi ya dawa hizo, hivyo wajue kuwa mapambano haya si ya mtu mmoja.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo