Mbowe amburuta Makonda kortini


*Awashitaki pia Kamanda Sirro na Mpelelezi Mkuu Wambura
*Awakilishwa na Kurugenzi ya Haki za Binadamu ya Chadema

Waandishi Wetu

Freeman Mbowe
KIONGOZI wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, amekwenda mahakamani kufungua kesi ya kikatiba dhidi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Taarifa iliyopatikana jana ilisema Mbowe alifungua kesi hiyo dhidi ya Makonda, Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Camilius Wambura na Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Simon Sirro.

Kesi hiyo ilisajiliwa kama kesi ya kikatiba namba moja ya mwaka 2017 kwenye Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala ya Katiba (Masjala Kuu).

Katika kesi hiyo kwa mujibu wa chanzo cha habari, Mbowe anaiomba Mahakama Kuu itamke kuwa Mkuu wa Mkoa hana mamlaka ya kudhalilisha na kukamata.

“Mbowe pia ameiomba mahakama itengue vifungu vya 5 na 7 vya Sheria ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa kuwa ni batili na vinakiuka haki za Katiba,” kilisema chanzo cha habari hii.

Katika kesi hiyo, ilielezwa kuwa Mbowe anawakilishwa na mawakili kutoka Kurugenzi ya Katiba, Sheria na Haki za Binadamu ya Chadema.

Tuhuma

Juzi Makonda alimtaja Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai, kuwa mmoja wa watu 65 wanaotuhumiwa kujishughulisha na dawa za kulevya, akimtaka kuonana naye jana kwenye Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam kwa mahojiano.

Akizungumza jana mjini hapa na waandishi wa habari kabla ya kufungua kesi hiyo, Mbowe alisema hatakwenda kuonana na Makonda na badala yake atamburuta mahakamani kwa kumchafua.

Alisema atakwenda Polisi pale tu atakapopewa mwito maalumu wa kisheria unaomtaka kufika kituoni hapo kutokana na tuhuma hizo.

Mbowe, aliuita mwito huo wa Makonda kwake kuwa ni wa kijinai hivyo hawezi kuutii mpaka utakapokuwa wa kisheria.

“Nina mambo matatu ya kuzungumza; kwanza, nakanusha kwa nguvu zote kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya, kwa sababu katika maisha yangu, sijawahi kujihusisha na biashara hiyo au hata kutumia dawa za kulevya,” alisema Mbowe.

“Pili, sisi wapinzani, tunakubaliana na mapambano dhidi ya dawa hizo kwa sababu ni hatari kwa maisha yetu na tunaona vita hivi vilitakiwa vipiganwe miaka mingi iliyopita, lakini kutokana na sababu mbalimbali, havikupiganwa,” alisema.

Jambo la tatu kwa mujibu wa Mbowe ni kwamba Makonda si polisi na kwa mujibu wa sheria hana mamlaka ya kuita mtu Polisi ingawa ni kiongozi wa mkoa.

Alisema yeye ni Mbunge na kiongozi wa chama kikuu cha Upinzani, ni baba mwenye mke na watoto, hivyo hawezi kukubali ‘mjinga’ mmoja amchafue bila sababu.

“Who is (ni nani) Makonda? … siwezi kwenda Polisi kuhojiwa hadi watakaponiita kwa kufuata utaratibu wa kisheria. Kwa hiyo, nitamfungulia mashitaka ya kunikashifu wiki ijayo yeye kama yeye na  si kama Jamhuri kwa sababu sina tatizo na Jamhuri,” alisema.

“Katika hili, nitadai haki yangu katika mahakama za ndani na ikibidi za nje. Makonda hana fedha za kunilipa kutokana na alivyonichafulia jina,” alisema Mbowe.

Alisema atamfungulia mashitaka si kwa sababu ana shida na fedha, bali kutokana na kuchafuliwa jina.

Huku akifuatana na wabunge takribani 30 wa Upinzani, Mbowe alisema: “Nimejenga sifa yangu kwa miaka mingi na nitaendelea kuilinda kwa nguvu zote. Mimi si mtoto mdogo na hili ndilo tatizo la kuwapa watu vyeo wasio na busara.

“Kamwe huwezi kupambana na dawa za kulevya kwa kutaka sifa, nitamshitaki kwa sababu yeye ndiye ana kiherehere,” alisema.

Alisema hakuna anayemwogopa Makonda, kwa sababu tu yuko karibu na Rais John Magufuli na kusisitiza kuwa hana fedha ya kumlipa.

Akizungumzia utaratibu unaotumiwa na Makonda kutaja wahusika wa dawa za kulevya, alisema haufai kwa sababu unawafanya waanze kuchukua hadhari.

Alisema ana wasiwasi na wanaotajwa kwa maelezo kuwa baadhi yao wakiwamo walioelezwa kuwa wamiliki wa Yatch Club na Sleep Way, “hayo maeneo si ya mtu mmoja, yanamilikiwa kwa ubia na watu wengi.”

Akizungumza kwenye mkutano huo, kiongozi mkuu wa ACT-Wazalendo na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe alisema kama Mbowe angekuwa anajihusisha na dawa za kulevya, yeye angekuwa mshirika wake, kwa sababu amefahamiana naye tangu akiwa mdogo.

Alimpongeza kwa kugoma kwenda kuhojiwa Polisi. “Ningemshangaa kama angekwenda, maana Makonda hana mamlaka hayo. Makonda aseme ni sheria ipi inampa mamlaka ya kutangaza watu na kuwataka wakaripoti Polisi.”

Alibainisha kuwa anaposhambuliwa Mbowe ni sawa na kushambuliwa wapinzani wote na kubainisha jinsi alivyoibuliwa kwenye siasa na Mwenyekiti huyo wa Chadema.

Mwanzoni mwa wiki, Makonda aliitisha mkutano na waandishi wa habari  Dar es Salaam na kutaja watu 65 aliodai wanajihusisha na dawa za kulevya.

Pamoja na Mbowe, wengine ni Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, Mbunge wa zamani wa Kinondoni, Idd Azzan na mfanyabiashara Yusuf Manji.

Sirro

Baada ya kauli ya msimamo wa Mbowe, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Sirro jana alitangaza kwamba Jeshi hilo litamtia nguvuni Mbowe asipotii agizo la kwenda kituoni hapo kuhojiwa.

Kamanda Sirro alisema hayo wakati akijibu swali aliloulizwa na waandishi wa habari, uamuzi wa Mbowe kukataa kuripoti kituoni hapo kama alivyotakiwa na Makonda.

Kwa mujibu wa Kamishna Sirro, Jeshi hilo litahakikisha linamfuata kokote aliko, kwa kukaidi mwito wa kuhojiwa, ili kupata ukweli kuhusu kutajwa kuhusika na dawa hizo.

Alisema kwa kawaida mwenye hekima na busara hutii amri kwa kuitika mwito akiitwa, lakini akikaidi lazima achukuliwe hatua, hivyo kama Mbowe amekaidi alisema sheria itachukua mkondo wake.  

“Kama ikitokea mawakili na wanasheria wake wakaleta taarifa zenye sababu za msingi za kutoripoti tutamwacha na kumhoji hata kesho (leo) kwani lengo letu ni kumhoji ili kujua ukweli, lakini kama ameamua kukaidi msimamo wetu uko palepele,” alisema Kamanda Sirro. 

*Imeandikwa na Fidelis Butahe, Dodoma na Celina Mathew, Dar


Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo