Maalim akataa katakata kukutana na Lipumba


Christina Mseja

Lipumba na Maalim Seif
KATIBU Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, amesisitiza kuwa haoni sababu ya kukutana na Profesa Ibrahim Lipumba kuzungumzia mambo ya chama kwa kuwa si mwanachama halali wa CUF hivi sasa.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana, ilisema Maalim Seif alitoa kauli hiyo kwenye ziara ya siku nne kwenye wilaya saba za mikoa mitatu ya Unguja.

Maalim alisema ataendelea kufuata taratibu za kisheria ili kuhakikisha chama kinamaliza moja kwa moja mgogoro aliodai umepandikizwa na CCM kupitia kwa Lipumba.

Alitaka wapenzi na wanachama wa CUF kuunga mkono jitihada   zinazofanywa na chama kupigania demokrasia ya kweli nchini.

Aliwataka wanachama wa CUF kushirikiana na viongozi wakuu wa CUF wanaotambuliwa na Baraza Kuu la Uongozi kujenga na kuimarisha chama hicho.

Alifafanua kuwa wakati anaendelea kuimarisha chama kupitia viongozi halali, ni vema wasiwe na wasiwasi na uamuzi walioufanya kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 mwaka juzi kwa kuipa CUF ushindi wa urais wa Zanzibar kuwa hautapuuzwa.

Aliwataka kuendelea kuwa watulivu na kuwahakikishia kuwa siku chache zijazo haki yao itapatikana. "Nawahakikishia, tumepigana vya kutosha katika kudai haki yetu na tumefikia hatua nzuri za kupata haki yenu.

“Hatua ya wananchi wa Zanzibar ya kuipa ushindi CUF ni kutokana na CCM kushindwa kuongoza Wazanzibari kwa misingi ya haki, usawa na demokrasia,” alisema.

Alifafanua kuwa mgogoro wa uongozi ndani CUF uliotokana na hatua ya Profesa Lipumba kuamua kurudi katika nafasi ya uenyekiti wa chama hicho na kusema watahakikisha wanapata ushindi.

“Lipumba alijiuzulu mwenyewe hivyo hakuna hoja yoyote ya kisheria inayomwezesha kurudi tena katika nafasi hiyo,” alisema.

Maalim Seif ataendelea na ziara hiyo katika Wilaya ya Magharibi ‘A’, ‘B’ kisiwa cha Unguja, Pemba hadi Februari 24.

Pamoja na kufanya ziara hiyo na kuzungumza na viongozi wa chama na jumuiya zake, Katibu atafanya uzinduzi na uimarishaji wa waratibu wa chama.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo