Majaliwa aagiza viongozi waende Engusero


Mwandishi Wetu, Kiteto

Kassim Majaliwa
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewaagiza Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Tumaini Magesa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Tamim Kambona kwenda kata ya Engusero keshokutwa kufanya mkutano wa hadhara na kujibu kero za wananchi wa kata hiyo.

Viongozi hao wametakiwa pia wafuatane na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Lairumbe Mollel wakatoe ufafanuzi bila kukosa.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana kijijini Engusero wilayani hapa baada ya kusimamishwa na wananchi akiwa njiani kwenda Kibaya yaliko makao makuu ya wilaya hii kuanza ziara ya kikazi mkoani Manyara.

Akijibu baadhi ya maswali aliyoulizwa na wananchi wa Engusero, Waziri Mkuu alichukua ombi la wakazi hao la kujengewa soko la kimataifa ili wauze mahindi yao hapo hapo.

“Nitaawagiza Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Halmashauri waje hapa Jumamosi hii na kufanya mkutano ili wawaeleze wana mpango gani kuhusu soko hilo,” alisema.

Awali, mkazi wa kata hiyo, Ali Athumani alimwomba Waziri Mkuu awasaidie ili kujengewa soko la kimataifa kwa sababu wao ni wazalishaji wakubwa wa mahindi, lakini hawafaidiki nayo kwa sababu yote yanauzwa soko la Kibaigwa.

Said Shabani alimwomba Waziri Mkuu awasaidie kufuatilia upatikanaji gari la wagonjwa na ujenzi wa wodi nyingine ya na mochari kwenye zahanati yao.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alisema Serikali imeweka nia ya dhati ya kupambana na dawa za kulevya na kuwataka watendaji wote kuanzia ngazi ya vijiji wadhibiti kadhia hiyo.

“Tunataka vijiji vyetu, kata zetu, wilaya zetu na mikoa yetu iwe safi bila hata chembe ya dawa za kulevya. Tukikuona kijana unayumbayumba au kuweweseka, tunakupima na tukikuta umetumia ile kitu, tunakukamata ili utwambie nani amekupa,” alisema na kuongeza:

“Sisi tunataka vijana wafanye kazi za kujiletea maendeleo. Kijana hawezi kuwa na maendeleo wakati hafanyi kazi, hawezi kuwa na ndoto za maendeleo wakati amelewa bangi au dawa za kulevya. Kila mmoja afanye kazi kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu,” alisisitiza.

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo